Duale ashtumu Jubilee kwa kuzamisha Kenya kwa madeni

Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale. Picha Maktaba
Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale. Picha Maktaba

Serikali ya rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto itakumbukwa kwa kuzamisha taifa la Kenya katika lindi la madeni.

Akizungumza katika mahojiando ya kipekee kwenye Citizen TV, aliyekuwa kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Aden Duale kwa mara ya kwanza amekiri kwamba serikali ya Jubilee itawacha taifa la Kenya katika dimbwi la madeni na huenda itakuwa vigumu kulipa madeni hayo ikiwa serikali haitashauriana na wale iliyowakopa ili kuratibu madeni hayo upya.

Mbunge wa Garissa Mjini na ambaye alikuwa akisimamia shughuli za serikali katika bunge kwa takriban miaka saba alikiri kwamba rais Uhuru Kenyatta alipotoshwa na washauri wake kuhusiana na maswala kadhaa ya kifedha.

Licha ya kwamba serikali ya Jubilee ilifanya vyema katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza uongozini, Duale alisema wazi kwamba serikali ya Uhuru na Ruto ilikopa pesa kuliko uwezo wa taifa kulipa kwa urahisi.

Rais Uhuru Kenyatta (kulia) na naibu wake Williama Ruto
Rais Uhuru Kenyatta (kulia) na naibu wake Williama Ruto

Alisema huenda aliyekuwa waziri wa fedha Henry Rotich na kikosi chake walikosa kumshauri vyema rais kuhusu maswala ya kifedha hasa kuhusu kiwango cha ukopaji wa fedha kwa miradi mbali mbali ya kitaifa.

Daule kwa mara ya kwanza alifichua sababu iliyopelekea Kenya kukopa pesa nyingi kutoka Uchina, alisema kwamba baadhi ya viongozi wafisadi na wafanyibiashara wenye ushawishi mkubwa walichochea taifa kuchukuwa mikopo ya uchini yenye riba za juu kwa sababu walikuwa wakipewa asilimia 10 kwa mikopo hiyo.

Mbunge huyo hata hivyo alikataa kutaja majina ya wahusika akisema kwamba wanajulikana.

Kuhusiana na hali ya sasa ya kifedha ya taifa, Duale alisema kwamba alilazimika kuomba bunge kuongeza kiasi cha pesa ambazo serikali inafaa kukopa hadi shilingi trilioni tisa baada ya waziri mpya wa fedha Ukur Yattani kueleza masaibu ambayo serikali ilikuwa inapitia huku ikijaribu kulipa madeni ya awali.

Alisema kama bunge halingekubali serikali kuongeza kiwango cha ukopaji basi Kenya ingejipata pabaya na huenda ingeshindwa hata kulipa madeni ya sasa na yale ambayo muda wa kulipa ulikuwa umewadia.

Mbunge huyo alitaja mradi wa tarakilishi kwa shule za msingi kama moja wapo wa miradi ambayo serikali ilipotoshwa kuanzisha. Alisema kulikuwa na mambo mengine ambayo yangepewa kipau mbele kwanza katika sekya ya elimu kabla ya kuanza kufikiria mambo ya kuwapa wanafunzi tarakilishi.

Duale alisema kwamba hajutii kuhudumu kama kiongozi wa wengi katika bunge na kwamba anajivunia mafanikio yake.

Mbunge huyo aling’atuliwa kutoka wadhifa huo mwaka huu na wadhifa wake kuchukuliwa na mbunge wa Kipipri Amos Kimunya.