Hofu baada ya jeneza lililokuwa na konokono, kuku hai kupatikana limetupwa kwa mtu Kisumu

Ndani ya jeneza hilo palikuwa na konokono, kuku hai aliyekuwa amefungiliwa rozari shingoni mwake pamoja na bidhaa zingine za kutisha.

Muhtasari

•Hofu ilitanda katika kijiji cha  Kogony Korando kilicho katika kaunti ya Kisumu baada  ya jeneza ndogo kupatikana likiwa limeachwa katika nyumba moja maeneo hayo.

•Mwenye nyumba husika  Silvestor Okello alisema kuwa waliona jeneza hilo walipoamka asubuhi

•Okero alisema kuwa hana shida na mtu yeyote ila alishuku kuwa huenda ni jamaa wake wa karibu ambaye wamekuwa wakizozania shamba alitekeleza kitendo hicho cha kichawi.

Jeneza lililopatikana Kisumu
Jeneza lililopatikana Kisumu
Image: FAITH MATETE

Hofu ilitanda katika kijiji cha  Kogony Korando kilicho katika kaunti ya Kisumu baada  ya jeneza ndogo kupatikana likiwa limeachwa katika nyumba moja maeneo hayo.

Ndani ya jeneza hilo palikuwa na konokono, kuku hai aliyekuwa  amefungiliwa rozari shingoni mwake  pamoja na bidhaa zingine za kutisha.

Mwenye nyumba husika  Silvestor Okello alisema kuwa waliona jeneza hilo walipoamka asubuhi.

Okero alisema kuwa alipigwa na butwaa na kuita jirani aje ashuhudie maajabu yale pia.

"Jeneza hilo lilikuwa limefungwa na sikulifungua. Niliita jirani yangu aje anisaidie"  Okero alisema.

Okero alisema kuwa hana shida na mtu yeyote ila alishuku kuwa huenda ni jamaa wake wa karibu ambaye wamekuwa wakizozania shamba alitekeleza kitendo hicho cha kichawi.

Jirani aliyeitwa kushuhudia alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Riat na baada ya hapo  jeneza lile likafunguliwa.

Inaripotiwa kuwa chifu wa eneo hilo ndiye alifungua jeneza lile kabla ya mashahidi waliokuwa pale kupatwa na mshangao mkubwa baada ya kuona kilichokuwa ndani.

"Ni jambo la kusikitisha sana. Baada ya kufunguliwa niliona kuku mweusi sana. Sijwahi kuona kitu kama kile maishani mwangu. Niko na miaka hamsini sasa" Jirani huyo alisema.

Alisema kuwa baada ya jeneza kufunguliwa, liliondolewa nyumbani pale na kuenda kuchoma kila kitu kilichokuwa ndani.