Safaricom kuongeza bei za simu kwa 10% na laini kwa Ksh 50 zaidi kuanzia Julai 15.

Ongrzeko hili ni kutokana na amri ya serikali kuongeza ushuru kwa bidhaa hizo za kielektroniki

Muhtasari

• Safaricom ilitangaza kuongeza bei za simu kwa asilimia kumi ili kuafikia tozo la ushuru kutoka kwa serikali.

• Pia kampuni hiyo ilisema bei za laini za simu ambazo kwa sasa zinauzwa shilingi 50 zitaongezwa kwa shilingi nyingine 50 zaidi.

Laini za Simu na simu
Laini za Simu na simu
Image: Maktaba (The Star)

Kampuni ya mawasiliano ya Safaricom imetangaza kuwa kuanzia Ijumaa leo hii bei za laini za simu pamoja na simu zenyewe zitapanda kama njia moja ya kuafikia ongezeko la tozo la ushuru ambalo serikali ya Kenya imeweka kwa bidhaa hizo.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti moja la biashara humu nchini, Safaricom walisema simu mpya zitaongezewa bei kwa angalau asilimia 10 na laini za simu kuongezewa bei kwa shilingi 50 zaidi ya bei ya sasa.

Safaricom wanasema mabadiliko hayo ya bei za bidhaa za kielektroniki ni kutokana na ongezeko la tozo ambalo serikali iliweka kwa bidhaa hizo kuanzia mwanzo wa mwezi Julai.

“Kuanzia tarehe 15 Julai 2022 tutakuwa tutaongeza bei yetu ya kadi za simu hadi Sh50 pamoja na mjazo wa vocha wa Sh50 kwa mtumizi wa kwanza ili kujumuisha ushuru wa bidhaa. Bei za simu zitaongezwa ili kujumuisha asilimia 10 ya ushuru wa bidhaa na asilimia 25 ya ushuru wa forodha kwa vile viwango vilivyopo vya hisa vitabadilishwa na kuweka hisa mpya ambapo ushuru mpya utatumika,” gazeti hilo lilinukuu taarifa ya Safaricom.

Mabadiliko haya ya bei za bidhaa za simu yanakuja wakati ambapo Wakenya tayari wanazidi kupitia wakati mgumu kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha na bei za bidhaa za kawaida kama vile unga wa mahindi, mafuta ya kula, maziwa, sabuni miongoni mwa bidhaa zingine zenye umuhimu mkubwa zikiendelea kutorokea paani, Wakenya wasijue jinsi ya kukidhi na kujikimu kimaisha.