Polisi kuchunguza tukio la dereva kukaidi amri ya kusimama

Huduma ya polisi ilisema polisi wanafua mstari wa mbele kuimarisha usalama barabarani.

Muhtasari

•Polisi walionekana wakilizuia gari la aina ya Saloon bila mafanikio huku polisi mmoja akimnyooshea kidole dereva.

•NPS ilisema kuwa suala hilo kwa sasa linachunguzwa na kwamba hatua zinazofaa za kurekebisha zitachukuliwa mara moja.

Idara ya Huduma kwa polisi (NPS) imelaani tukio ambapo dereva wa gari ndogo alinaswa katika video akiwashirikisha  maafisa wa trafiki waliokuwa wakimkimbiza katika mchezo wa paka na panya.

Katika video hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, gari la kijani lenye nebo ya NTSA linaonekana likajaribu kulizuia gari la aina ya Saloon bila mafanikio huku polisi mmoja akimnyooshea kidole dereva.

Dereva huyo alipoagizwa kusimama alipuuza, akasonga kando kisha kuendelea na safari bila kujali matokeo ya matendo yake.

Polisi wamesisitiza kuwa madereva wanafaa kuwa watu makini na waangalifu wanapokuwa barabarani.

"Tunakubali sababu ya usalama barabarani ni kukuza umakinifu na uwajibikaji tukiwa kwenye barabara za umma, na haya ni matarajio ya kimsingi yaliyowekewa madereva wote wa magari na watumiaji wa barabara, bila kuwasaza maafisa wa usalama," NPS ilieleza kwenye ukurasa wao wa Facebook siku ya Alhamisi.

NPS ilisema kuwa suala hilo kwa sasa linachunguzwa na kwamba hatua zinazofaa za kurekebisha zitachukuliwa mara moja.

"Tunapoendelea kukagua tukio kwa hatua za kurekebisha, tunalaani tabia hiyo ya kutowajibika," NPS ilihakikisha.