KNH: Miili 217 ya watoto ni kati ya ile itakayozikwa kwenye kaburi la pamoja

Usimamizi wa hospitali ya KNH ulitoa makataa ya siku 21 kwa miili 233 kutambuliwa na kuchukuliwa la sivyo itazikwa kwenye kaburi la pamoja.

Muhtasari

• Kinachoshangaza ni kwamba kati ya miili hiyo 233, miili 217 kati yao ni ya watoto huku mingine ikiwa ya watu wazima.

Majeneza yaliyobeba mabaki ya miili ya watoto walioaga dunia
Majeneza yaliyobeba mabaki ya miili ya watoto walioaga dunia
Image: Maktaba

Hospitali ya kitaifa ya Kenyatta Alhamisi ilitangaza mpango wa kuzika miili zaidi ya 200 iliyotelekezwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo kwa muda mrefu.

Katika taarifa iliyotolewa kwa umma na ambayo ilionekana na vyombo vya habari, miili ambayo bado haijawahi chukuliwa na wenyewe ni 233 na ambayo sasa usimamizi wa hospitali ya Kenyatta umetoa makataa ya siku 21 kwa umma au mtu yeyote aliyempoteza mpendwa wake kufika katika makafani ya KNH Nairobi ili kuitamua miili hiyo na kuichukua, la sivyo itazikwa katika kaburi la pamoja.

Kinachoshangaza ni kwamba kati ya miili hiyo 233, miili 217 kati yao ni ya watoto huku mingine ikiwa ya watu wazima.

Kulingana na orodha iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa KNH Evanson Kamuri, watoto ndio kundi lililoathiriwa zaidi na tatizo hili linaloonekana kukua. Wengi hufia hospitalini kila mwezi lakini miili yao haidaiwi kamwe.

Usimamizi wa hospitali hiyo ulitetea hatua yao ya kutaka kuizika miili hiyo katika kaburi la pamoja baada ya siku 21  zijazo kwa sababu wanataka kupata nafasi ya kuhifadhi miili mingine mipya.

Itakumbukwa mwezi jana serikali ya kaunti ya Nairobi pia ilichukua uamuzi wa kuizika miili 236 katika kaburi la pamoja baada ya kukosekana kutambuliwa na wenyeji kwa muda mrefu. 218 kati ya miili hiyo ilikuwa imetelekezwa katika makafani ya City huku 18 ikiwa katika makafani ya hospitali ya Mama Lucy.