Tumia bunduki zetu kukabiliana na magenge hatari - rais Ruto awaambia polisi

Tusingoje maafisa wetu wakauawe na wakora, ni sharti tukabiliane na wakora kabla hawajakabiliana na maafisa wetu - Ruto.

Muhtasari

• Kama afisa yeyote ako hatarini ya majambazi, ni lazima atumie silaha yake kukabiliana na majambazi. - Ruto.

Rais Ruto na maafisa wa polisi
Rais Ruto na maafisa wa polisi
Image: STAR

Rais William Ruto amewapa mamlaka mia kwa mia maafisa wa polisi kutumia silaha zao za ulinzi kukabiliana na magenge ya ujambazi ambayo yameripotiwa kuwahangaisha mamia wa wakaazi katika baadhi ya miji tajika nchini Kenya.

Wakati wa mkutano wa Jumatano, Novemba 16 na makamanda wakuu wa polisi, mkuu wa nchi aliwahimiza maafisa hao wasisite kutumia bunduki zao. Ruto alisema serikali haitaruhusu magenge ya wahalifu kuteka miji ya Kenya au sehemu nyingine yoyote ya taifa.

“Serikali ya Kenya itamlinda kila afisa wa umma na kila polisi ambaye anafanya kazi yake kwa njia sahihi. Kwa hiyo nawataka mwalinde wote, haswa watu wa kawaida, sisi wengine tunaweza kujilinda. Acha tupigane na majambazi, wezi na nawaambia katika hio tutawaunga mkono. Hatuwezi kubali magenge ya majambazi kutawala miji yetu au hata sehemu yoyote ya Kenya. “

“Tumewapa silaha, sheria iko upande wenu, kuhakikisha kwamba mnakabiliana na majambazi kwa njia stahiki. Kama afisa yeyote ako hatarini ya majambazi, ni lazima atumie silaha yake kukabiliana na majambazi. Tusingoje maafisa wetu wakauawe na wakora, ni sharti tukabiliane na wakora kabla hawajakabiliana na maafisa wetu,” rais Ruto aliwaambia walinda usalama.

Vile vile, rais alizitaka idara zote za usalama kufanya kazi kwa uadilifu pasi na kujihusisha na mambo ya kisiasa bali kuwahakikishia wananchi wote usalama kwa usawa pasi na kuangalia wanaegemea mrengo upi wa kisiasa.

“Polisi hawana ruhusa na kujihusisha na mambo ya kisiasa. Usichukue mrengo wowote wa kisiasa. Tuna watu wa kutosha kutusaidia katika masuala ya kisiasa. Tuna waendeshaji wa vyama vya kisiasa, tuna wanaharakati, na watu wengine wote. Tunataka polisi kuwa huru kutokana na mwingilio wa mrengo wowote na kumlinda kila mwananchi bila kuangalia ni mrengo upi wa kisiasa anaegemea,” rais Ruto alifoka.

“Haijalishi, nataka mwalinde ndugu zetu walioko upinzani njia sawa na mnavyowalinda wale walio upande wa serikali kwa sababu sisi wote ni watu wamoja na tunalipa ushuru.”