Noordin Haji: Kwa nini siwezi taja thamani ya utajiri wangu

Haji alisukumwa kutaja thamani ya utajiri wake lakini akakataa akisema kuwa ingekuwa vyema akituma majumuisha kwa kamati pekee na wala si kwa umma,

Muhtasari

• Ikumbukwe wiki mbili zilizopita rais Ruto alimteua Haji katika wadhifa wa mkuu wa NIS

• Alipofika bungeni, moja ya maswali ya msingi ambayo alikabiliwa nayo ni kutaja kutaja kima cha utajiri wake.

Noordin Haji akataa kutaja thamani ya utajiri wake
Noordin Haji akataa kutaja thamani ya utajiri wake
Image: Maktaba

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji alasiri ya Jumanne alifika mbele ya kamati ya bunge ya idara ya ulinzi, upelelezi na mahusiano mema ya nje kuhojiwa kuhusu ufaafu wake kuchukua nafasi kama mkurugenzi mkuu wa ujasusi, NIS.

Ikumbukwe wiki mbili zilizopita rais Ruto alimteua Haji katika wadhifa wa mkuu wa NIS na alipofika bungeni, moja ya maswali ya msingi ambayo alikabiliwa nayo ni kutaja kutaja kima cha utajiri wake.

Hata hivyo, Haji alizua minong’ono bungeni alipokataa kabisa kutaja thamani ya utajiri wake akisema kuwa suala hilo ni la kiusalama Zaidi kutokana na hali ya kazi ambayo analenga kukabidhiwa baada ya kupita mchakato wa mahojian hayo

Haji alisema kuwa thamani yake inaweza kuwa suala la "usalama wa taifa" katika siku za usoni iwapo atafanikiwa kupata kazi hiyo, hivyo afadhali asifichue hadharani.

Haji alijibu: “Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba, kwa kuzingatia unyeti wa ofisi nitakayoshika, kwamba nitoe hili kwa kamati...laweza kuwa suala la usalama wa taifa wakati fulani.”

Aliposhinikizwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Nelson Koech kueleza utajiri wake kwa madhumuni ya kuwa kwenye rekodi, DPP badala yake aliomba aruhusiwe kuwasilisha majumuisho ya mapato yake ya kifedha kwa kamati pekee na wala si kuyataja waziwazi mbele ya vyombo vya habari.

Mbunge wa Kinangop Thuku Kwenya alizidi kumchukua DPP kuwajibika kuhusu sehemu maalum ya majibu yake, ambayo alichukua kuashiria kuwa Haji alikuwa na uhakika wa kupitia mchakato wa uhakiki na kushika wadhifa kama bosi mpya wa NIS.

“Nimemsikia mteule akisema ‘ofisi nitakayoshika’...ni kana kwamba umemaliza shughuli zetu na kwa hiyo tujitokeze twende tu,” alisema Kwenya.

Haji alisema: “Pole, labda ni uangalizi tu, kama mtaniruhusu (kushika ofisi). Naomba radhi kama ndivyo ilivyotokea.”