Mlipuko wa gesi Embakasi: Ruto aamuru kufutwa kazi kwa maafisa waliotoa leseni

Mkuu huyo wa Nchi aliagiza kuwa Wizara ya Nishati ihakikishe watu wanaohusishwa na suala hilo wanapaswa kuondoka mara moja na kushtakiwa kwa makosa waliyofanya.

Muhtasari

• Alieleza wasiwasi wake kuwa watu serikalini wametoa leseni za biashara hiyo kuendeshwa katika makazi ya Wakenya wakihatarisha maisha yao.

Moto Embakasi
Moto Embakasi
Image: Ezekiel Aming'a//THE STAR

Rais William Ruto ameamuru kufutwa kazi kwa maafisa wa serikali wanaoshutumiwa kwa kutoa leseni kinyume cha utaratibu wa utendakazi wa kiwanda cha gesi ambacho kilisababisha mlipuko Ijumaa asubuhi.

Akizungumzia suala hilo mjini Lugali Jumamosi asubuhi, Ruto alihusisha kisa hicho na ufisadi, ukosefu wa uadilifu, na uroho miongoni mwa maafisa wa serikali waliohusika kumpa leseni mhudumu.

Mkuu huyo wa Nchi aliagiza kuwa Wizara ya Nishati ihakikishe watu wanaohusishwa na suala hilo wanapaswa kuondoka mara moja na kushtakiwa kwa makosa waliyofanya.

Alieleza wasiwasi wake kuwa watu serikalini wametoa leseni za biashara hiyo kuendeshwa katika makazi ya Wakenya wakihatarisha maisha yao.

"Nataka niseme ili kuepusha mashaka, viongozi wa serikali waliotoa leseni za uwekaji gesi kwenye makazi ya watu wakati ilionekana wazi kuwa ni kosa, lakini kwa sababu ya uzembe na ufisadi walitoa leseni,"

Aliendelea: “Leo tuna majeruhi, tuna Wakenya ambao wamefariki, wale wenzetu waliohusika katika hili, lazima wizara ichukue hatua mara moja dhidi yao na lazima wafukuzwe kazi na kufunguliwa mashtaka kwa uhalifu waliofanya.

Rais alisema hakuna haja ya watu hao kuendelea kushikilia ofisi za serikali na kulipwa kwa fedha za walipa kodi.

Ijumaa jioni, serikali ilitangaza mipango ya kukabiliana na ghala za kuhifadhi na kujaza gesi nchini baada ya mojawapo kushika moto huko Embakasi Ijumaa asubuhi.

Watu watatu wamefariki dunia na wengine zaidi ya 280 kujeruhiwa kufuatia tukio eneo la Mradi baada ya mtambo wa kujaza na kuhifadhi gesi kuwaka moto.

Katika taarifa ya pamoja, Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki na mwenzake wa Kawi Davis Chirchir walisema serikali itabomoa maeneo yote haramu kupitia Mpango wa Matokeo ya Haraka wa Mashirika mengi.

"Serikali itatumia hatua za kiutawala za kuadhibu kwa waendeshaji wote wa Gesi ya Kimiminika ya Petroli (LPG) watakaopatikana wakijaza mitungi bila mamlaka ya maandishi ya wamiliki wa chapa," CS Kindiki alisema.

Alisema serikali itahakikisha tathmini mpya ya hatari inafanywa kwa mitambo yote ya LPG nchini kwa nia ya kufunga maeneo yote yasiyokidhi viwango.

Muungano wa Vyama vya Wakazi nchini Kenya umeshutumu serikali kwa kukosa kutekeleza sheria na kanuni ili kulinda umma dhidi ya hatari.