Raila atua Siaya kwa mazishi ya Fred Omondi

Raila ameandamana na Gavana wa Siaya James Orengo na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi miongoni mwa viongozi wengine wakuu wa ODM.

Muhtasari

• Raila anajitokeza hadharani kwa mara ya kwanza tangu Generation Z ilipochochea nchi kwa wimbi la maandamano ya kupinga mswada wa fedha.

• Ingawa Raila alitoa wito wa kukataliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024, hakutoa maoni yake kuhusu maandamano hayo.

KINARA WA UPINZANI RAILA ODINGA
Image: EZEKIUEL AMING'A

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga ametua katika kaunti ya Usenge Siaya kuhudhuria mazishi ya mcheshi Fred Omondi.

Fred ni kakake mcheshi maarufu na mwanaharakati Eric Omondi.

Fred alifariki katika ajali ya barabarani kwenye barabara ya Kagundo asubuhi ya Juni 15.

Polisi walisema ajali hiyo ilitokea baada ya bodaboda iliyokuwa imembeba Fred kuhusika katika kugongana uso kwa uso na basi la mwendo kasi mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi.

Raila ameandamana na Gavana wa Siaya James Orengo na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi miongoni mwa viongozi wengine wakuu wa ODM.

Raila anajitokeza hadharani kwa mara ya kwanza tangu Generation Z ilipochochea nchi kwa wimbi la maandamano ya kupinga mswada wa fedha.

Ingawa Raila alitoa wito wa kukataliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024, hakutoa maoni yake kuhusu maandamano hayo.

Hata hivyo, Raila alikashifu utumizi wa Serikali wa kutumia nguvu inayodaiwa kuwa ya kikatili dhidi ya waandamanaji.

“Nimesikitishwa na mauaji, kukamatwa, kuzuiliwa na ufuatiliaji unaofanywa na polisi kwa wavulana na wasichana ambao wanatafuta tu kusikilizwa kuhusu sera za kutoza ushuru zinazowaibia maisha yao ya sasa na ya baadaye,’’ Raila alisema kwenye taarifa.

''Tulitegemea kuwa serikali ingeonyesha nia njema na unyenyekevu na walau kuwasikiliza watoto wa nchi, Badala yake, kila maoni yanayopingana yametupiliwa mbali na kukejeliwa na viongozi wa serikali na wanasiasa wa chama tawala na sauti hizo zinazokinzana sasa zimezimwa na ukatili na unyama.'