SRC yapiga breki mpango wa nyongeza ya mishahara baada ya wanasiasa wengi kuipinga

Mwenyekiti wa SRC Lyn Mengich alisema tume iliamua kubatilisha mpango wa nyongeza wa mishahara baada ya kushiriki mashauriano ya umma.

Muhtasari

• Mwenyekiti wa SRC Lyn Mengich alisema tume iliamua kubatilisha mpango wa nyongeza wa mishahara baada ya kushiriki mashauriano ya umma.

 

Mwenyekiti wa SRC Lyn Mengich
Mwenyekiti wa SRC Lyn Mengich
Image: MATKTABA

Tume ya kuratibu mishahara na marupurupu ya wafanyikazi humu nchini, SRC imesitisha mpango wa nyongeza ya mishahara kwa wanasiasa na baadhi ya maafisa wa serikalini.

Nyongeza hiyo ya mishahara ilikuwa imeratibiwa kuanza kuteelezwa Julai mosi kufuatia notisi kwenye gazeti la serikali mwezi Agosti mwaka jana.

Hata hivyo, baada ya pingamizi kutoka kwa wananchi na baadhi ya wanasiasa ambao walijitenga na kuomba nyongeza hiyo, sasa tume hiyo imefutilia mbali mpango huo wa nyongeza.

SRC ilisema Jumatano kwamba "imesimamisha uhakiki wa nyongeza wa mishahara kwa maafisa wote wa serikali na itapitia ushauri kwa maafisa wengine wote wa umma ili kuhakikisha kuwa bili ya mishahara inamudu na uendelevu wa kifedha."

Mwenyekiti wa SRC Lyn Mengich alisema tume iliamua kubatilisha mpango wa nyongeza wa mishahara baada ya kushiriki mashauriano ya umma.

SRC ilikuwa imechapisha mawasiliano rasmi katika Gazeti la Kenya mnamo Agosti 2023 ya mpango wake wa kuongeza mishahara ya maafisa wa serikali kuanzia Julai 1, 2024.

Rais wa William Ruto aliagiza wizara ya fedha ya nchi hiyo kusimamisha nyongeza ya mishahara iliyopendekezwa.

Rais Ruto alisema hatua hiyo itasaidia Kenya "kuishi kulingana na uwezo wetu."

Baraza la magavana, chama cha magavana wote 47 wa Kenya, liliitaka SRC kuondoa mipango ya kuongeza mishahara ya maafisa wa serikali.

Kulingana na mapendekezo ya mishahara, mbunge angepokea nyumbani shilingi 739,600 kila mwezi, kutoka shilingi 725,500 za sasa.

Uamuzi wa kubatilisha mishahara iliyopendekezwa unajiri wakati wananchi wakiutaka utawala wa Rais Ruto kudhibiti ubadhirifu serikalini.

Maandamano ya hivi majuzi ya kupinga nyongeza ya ushuru nchini Kenya yaligharimu maisha ya takriban watu 39, kulingana na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNCHR) inayofadhiliwa na serikali.

Maandamano hayo yalimfanya Ruto kukataa Mswada wa Fedha wa 2024, ambao ulikuwa umependekeza ushuru wa juu.