Kama wapinzani rasmi, tutaijukumisha serikali ya Ruto - Wajackoyah

Wajackoyah alisema wao kama wapinzani, wataikosoa serikali ya Ruto pindi itakapoenda pabaya.

Muhtasari

• “Ni lazima pia tumshukuru Raila Odinga kwa kupigania demokrasia ambayo leo hii tunajivunia,” Wajackoayah alisema.

Mgombea urais Wajackoyah,wakati wa mahojiano na Radiojambo 10/juni/2022
Image: CHARLENE MALWA

Aliyekuwa mgombea urais kupitia tikiti ya chama cha Roots, wakili msomi George Wajackoyah amempongeza raia mteule William Ruto baada ya mahakama ya upeo kudumisha ushindi wake.

Wajackoyah amesema kwamba yeye kama mpinzani rasmi ataijukumisha serikali ya rais Ruto kwanzia sasa Kwenda mbele kwani maisha lazima yasonge.

“Kama mwanachama rasmi wa upinzani, tutaijukumisha serikali ya rais mteule William Ruto, tutampa ujasiri ambao anastahili ila popote atakapoenda kombo tutamwambia," Wajackoyah alisema.

Wajackoyah alisemac kwamba zaidi ya wapiga kura milioni sita ambao walimpigia Raila kura wanalia kwa sasa ila akawaomba kudumisha amani kwani huo ndio uamuzi wa mahakama.

Akizungumza nje ya lango la mahakama ya upeo pindi baada ya jopo la majaji saba kudumisha ushindi wa Ruto, Wajackoyah pia alionekana kumpongeza Raila kwa kuwa kiongozi jasiri wa muda mrefu aliyepigania uhuru wa kidemokrasia.

“Ni lazima pia tumshukuru Raila Odinga kwa kupigania demokrasia ambayo leo hii tunajivunia,” Wajackoayah alisema.

Wajackoyah pindi baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo ambao aliibuka wa tatu, paliibuka nyufa kubwa katika chama chake huku wakitofautiana vikali na aliyekuwa mgombea mwenza, Justina Wamae.

Wamae alikuwa anashuku kwamba Wajackoyah alikuwa anampigia debe kinara wa Azimio Raila Odinga chini ya zulia huku naye akitishia kujibwaga nyuma ya William Ruto.

Taarifa za wiki jana zilidai kwamab Wajackoyah tayari ashamtema Wamae na kumteua naibu mpya wa chama huku wakijiandaa kuvaa mawanda rasmi ya upinzani kama alivyodokeza.