Atwoli ampongeza Ruto baada ya ushindi wake kuidhinishwa na mahakama

Kwa muda mrefu Atwoli amekuwa mkosoaji mkubwa wa rais mteule William Ruto.

Muhtasari

•Atwoli alisema hatua ya kumpongeza Ruto baada ya hukumu ya mahakama ni uamuzi ambao ulifanywa wakati wa mkutano mkuu wa COTU.

•Mbunge wa zamani wa Nyeri Town Ngunjiri Wambugu pia amechukua hatua ya kumpongeza Ruto na kumtakia heri njema.

Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli.
Image: CHARLENE MALWA

Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyikazi nchini (COTU)  Francis Atwoli amempongeza rais mteule William Ruto kufuatia maamuzi ya Mahakama ya Upeo kuidhinisha ushindi wake.

Jumatatu alasiri mahakama ya upeo iliamua kwamba uchaguzi mkuu wa Agosti 9 ulikuwa halali na ulifuata sheria.

Katika taarifa yake baada ya hukumu hiyo, Atwoli alisema hatua ya kumpongeza Ruto baada ya hukumu ya mahakama ni uamuzi ambao ulifanywa wakati wa mkutano mkuu wa COTU.

"Wakati wa kikao cha  Bodi ya Uongozi  (K) mnamo tarehe 17 Agosti, tuliazimia kwamba mara tu baada ya uamuzi wa Mahakama ya Juu, lazima tumshukuru na kumpongeza mshindi. Kwa hivyo, tunampongeza Rais William Ruto," Atwoli alisema kupitia Twitter.

Bosi huyo wa COTU pia alichukua fursa hiyo kuwaomba wafanyikazi na Wakenya wote kwa ujumla kudumisha amani.

Kwa muda mrefu Atwoli amekuwa mkosoaji mkubwa wa Ruto. Amemkashifu hadharani mara nyingi na kumpigia debe mpinzani wake mkubwa Raila Odinga.

Mkosoaji mwingine mkubwa wa Ruto, mbunge wa zamani wa Nyeri Town Ngunjiri Wambugu pia amechukua hatua ya kumpongeza na kumtakia heri njema anapochukua jukumu lake mpya la kuongoza taifa.

"Hongera Rais William Ruto. Umeshinda dhidi ya uwezekano mkubwa sana. Sasa ninaomba kwa dhati ufanikiwe unapoliongoza taifa letu kuu la Kenya mbele. Sasa tunakusubiri kwa hamu #TimizaAhadi," Wambugu aliandika kwenye Facebook.

Mgombea mwenza wa Muungano wa  Azimio-One Kenya Martha Karua kwa upande wake amesema kuwa ingawa mahakama ya Upeo imeamua, hakubaliani kabisa na uamuzi ambao ulifanywa.