Ruto azungumza baada ya kushindwa kutumia Hustler Fund kulipa dau alilopoteza kwa mkewe

Rais William Ruto alipoteza dau kwa mke wake Rachel.

Muhtasari

•Rais alikuwa akiipigia upato timu ya Ufaransa kutokana na wingi wa wachezaji wenye asili ya Afrika kwenye kikosi hicho.

•Rais alitaka kuelewa ikiwa dau huendelea katika muda wa ziada baada ya mechi kuishia sare.

Image: RACHEL RUTO/TWITTER

Siku ya Jumapili, Rais William Ruto alipoteza dau kwa mke wake Rachel.

Wawili hao walikuwa wameweka dau ni nani angeshinda Kombe la Dunia, rais  Ruto akichagua Ufaransa huku Rachel akiichukua Argentina kunyanyua kombe hilo.

Rais alikuwa akiipigia upato timu ya Ufaransa kutokana na wingi wa wachezaji wenye asili ya Afrika kwenye kikosi hicho.

"Nashabikia timu ya Afrika katika fainali za Kombe la Dunia. Bahati nzuri Rachel na watoto mnapounga mkono upande mwingine. Kumbuka kulipa dau!! Kwa vyovyote vile natarajia mchezo mzuri wa soka," rais alisema kabla ya mechi.

Wakati mechi hiyo ikiendelea, huku Argentina wakiwa kifua mbele kwa mabao 2-0, Rachel alionekana kujiamini kushinda dau hilo.

"Mabao mawili mbele, dau bado lipo Bill?" Rachel alimuuliza mume wake kupitia mtandao wa Twitter.

Baada ya mechi kukamilika, Rachel alisherehekea ushindi wa Argentina na kumwagiza rais kulipa dau kama walivyokuwa wamekubaliana.

Ingawa matokeo hayakuwa kama jinsi alivyotarajia, Ruto pia aliipongeza Argentina  na kuahidi kulipa dau lake na mkewe.

"Hongera Argentina kwa kushinda Kombe la Dunia. Timu yangu ya Kiafrika kwenye Kombe la Dunia ilicheza mchezo mzuri sana. Nitalipa dau langu!!! Pande zote mchezo wa ajabu. Tukutane nyumbani," alisema.

Siku ya Jumatatu hata hivyo rais alidokeza kuwa bado hajatimiza ahadi yake kwa mkewe na kulalamika kwamba hapati amani nyumbani.

Alibainisha kwamba hakufanikiwa kutumia Hustler Fund kulipa deni hilo kwa kuwa fedha hizo zimepangwa kutumika kwa kazi tu.

"Hustler fund wamenikataza siwezi lipa bet nayo wanasema pesa ni ya husle. Isorait. Kwangu hakukaliki. Lady #1 na watoi ni pressure. Wale kuku zangu wataniokoa nilipe," rais alisema kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Hata hivyo,  kabla ya kulipa alitaka kuelewa ikiwa dau huendelea katika muda wa ziada baada ya mechi kuishia sare.