COFEK yaitaka KEBS kuondoa sokoni chapa ya unga unaojinadi kuwa hauna sumu ya aflatoxin

Shirikisho la kutetea ubora wa bidhaa kwa watumizi COFEK lilitaka mamlaka ya kukadiria ubora wa bidhaa KEBS kuchunguza chapa hiyo ya unga.

Muhtasari

• Baadhi ya Wakenya wamezua kwamab mahindi ambayo yamefika Mombasa bandarini ni ya GMO wakisema hawako tayari kununua mahindi hayo.

Unga wa mahindi kwenye rafu ya maduka makubwa.
Unga wa mahindi kwenye rafu ya maduka makubwa.
Image: MAKTABA

Shirikisho la kutetea watumizi wa bidhaa nchini Kenya COFEK limeitaka mamlaka ya kukadiria ubora wa bidhaa KEBS kuchunguza chapa moja ya unga ambao umeingia sokoni ukijinadi kwa kujitapa kuwa hauna chembechembe zozote za sumu ya aflatoxin.

Kupitia ukurasa wao wa Twitter, COFEK walisema kuwa kujinadi huko ni kwa kutiliwa shaka kwani wana maana ya ama hawana aflatoxin zozote au chapa zingine za unga zina chembechembe hizo za aflatoxin.

“Kwenu @KEBS_ke: Uwekaji chapa wa ajabu wa unga unaotiliwa shaka na usio wa kawaida (unga wa unga wa mahindi) unaoitwa '***' ni kukiuka kwa udanganyifu viwango vya uwekaji lebo. Uwekaji lebo hii unadai kuwa haina chembechembe zozote za aflatoxin au chapa zingine zina sumu,” sehemu ya tweet yao ilisoma.

Wasiwasi huu unakuja siku chache baada ya sehemu ya Wakenya kutaka serikali idhibitishe kama mahindi ambayo tayari yameagizwa kutoka nje ya nchi ni salama au ni mahindi ya GMO – mahindi ambayo wakenya wengi wameonekana kupinga wakidai kwamba wana habari mahindi ya GMO si mazuri kwa matumizi ya binadamu kama chakula.

Wikendi iliyopita, serikali ilidhibitisha kwamba meli ya kwanza iliyokuwa imebeba tani kadhaa za mahindi meupe imewasili katika bandari ya Mombasa na tayari mahindi hayo yameanza kusambazwa kwa wasagaji wa nafaka kote nchini, ikiwa na mpango wa rais Ruto kujaribu kupunguza bei ya unga wa mahindi na gharama ya juu ya maisha.

Msemaji wa ikulu Hussein Mohammed alinukuliwa akisema kuwa tayari mpango huo umeonekana kufaulu kwani unga umepungua kutoka bei ya Zaidi ya shilingi mia mbili kwa mfuko wa kilo mbili hadi shilingi mia sitini.

Lakini wakenya wengi wangali bado kupata unga wa bei hiyo ambayo Ruto alisema kwa kipindi cha wiki moja bei ya unga nchini ingepungua hadi shilingi 150 kwa pakiti ya kilo mbili.