Wanawake ndio kivutio kikuu cha utalii Kenya, acha kutoza vipodozi ushuru - MP Owino

Owino alisema kuwa hatua ya serikali kutoza ushuru bidhaa za urembo kutawafanya wanawake kuonekana vibaya hali ya kuwa wao ndio kivutio kikuu cha utalii humu nchini.

Muhtasari

• "Kivutio cha kipekee kwa watalii humu nchini ni wasichana wetu warembo. Kwa hiyo Kenya itapoteza mabilioni ya dola kwa sababu watalii watakoma kuja huku,” - Owino.

Babu Owino aikosoa serikali kutoza bidhaa za urembo ushuru.
Babu Owino aikosoa serikali kutoza bidhaa za urembo ushuru.
Image: Facebook

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ameisuta serikali ya Kenya Kwanza kwa hatua ya kutaka kutoza ushuru kwa bidhaa za urembo.

Owino alisema kuwa hatua hiyo ni sawa na kuwaibia watoto wa kike kwani asilimia kubwa ya bidhaa za urembo hutumiwa na wanawake.

“Serikali imepoteza mwelekeo, sasa inatoza ushuru kwa kila kitu. Sasa hivi wanatoza ushuru kwa mawigi, rangi za kucha, na hata ndevu bandia, vitu vyote ambavyo vinafanya vijana wetu kurembeka. Serikali ambayo inaiba kutoka kwa mabinti zetu si serikali nzuri. Mwanamume kamili hafai kuibia wanawake,” Owino alisema.

 Mbunge huyo mkereketwa wa sera za ODM alimsuta vikali rais Ruto akisema kuwa hatua hiyo itaifanya Kenya kupoteza mapato makubwa kutokana na sekta ya utalii kwani wanawake ndicho kivutio kikubwa cha utalii kwa sababu ya kupendeza kwao.

“Mabinti zetu wanavalia hizi bidhaa za urembo ili kuvutia watalii. Kivutio cha kipekee kwa watalii humu nchini ni wasichana wetu warembo. Kwa hiyo Kenya itapoteza mabilioni ya dola kwa sababu watalii watakoma kuja huku,” Owino alielezea.

Wiki jana wizara ya fedha ilitoa pendekezo kutaka bidhaa za urembo kuongezewa ushuru kama njia moja ya kuongeza pato la kitaifa ili kukidhi bajeti ya serikali, hatua ambayo hata hivyo imepata pingamizi kali kutoka kwa sehemu ya Wakenya ambao wanasema ushuru huo ni mzigo mzito kwa wananchi ambao tayari wamelazimika kubeba mzigo mzito wa ushuru katka bidhaa mbalimbali.