Kwa mara ya kwanza Raila anamtaja Ruto kama ''kaka yangu'' katika mazishi ya Mukami

Muhtasari

• Waziri huyo mkuu wa zamani amekuwa akimshambulia Ruto akisema hakushinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 dhidi yake.

Raila amtaja Ruto kama kakake katika mazishi ya Mukami
Raila amtaja Ruto kama kakake katika mazishi ya Mukami
Image: PSC

Kiongozi mkongwe wa upinzani Raila Odinga Jumamosi alimtaja Rais William Ruto kama ndugu na rafiki yake.

Hatua hiyo inaweza kuashiria kushuka kwa Raila ambaye ameendeleza mashambulizi dhidi ya serikali tangu uchaguzi uliopita.

Ukiweka tofauti za kisiasa kando, Raila alionekana kuutambua urais wa Ruto licha ya upinzani wake wa hapo awali dhidi ya serikali.

''Ndugu yangu William Samoei Ruto....'' Raila alisema huku akimtambua Ruto wakati wa mazishi ya Mama Mukami huko Kinangop, kaunti ya Nyandarua.

Waziri huyo mkuu wa zamani amekuwa akimshambulia Ruto akisema hakushinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 dhidi yake.

Licha ya tume ya uchaguzi kumtangaza Ruto kuwa mshindi wa uchaguzi huo na mahakama ya juu zaidi kuidhinisha ushindi huo, Raila amesisitiza kuwa alishinda uchaguzi huo.

Mnamo Jumamosi, Raila alionya serikali dhidi ya kuwakandamiza wananchi akisema kama walivyofanya wakati wa ukoloni, watatumia ghasia za kujihami kujilinda dhidi ya dhuluma.

''Polisi wanapotumia nguvu dhidi ya waandamanaji hiyo ni ghasia za uonevu na wananchi wanapopinga ukandamizaji unaoitwa vurugu za kujihami,'' Raila alisema.

Alisema wakati Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandera aliwekwa kizuizini, alizungumzia jinsi wananchi wanaweza kutumia upinzani wa kujihami kujilinda.