Polisi wavamia nyumba za aliyekuwa kiongozi kundi la Mungiki Njenga

Alihusisha uvamizi huo na ibada ya mazishi iliyopangwa ya mke wa Dedan Kimathi

Muhtasari

• Alihusisha uvamizi huo na ibada ya mazishi iliyopangwa ya mke wa Dedan Kimathi, Field Marshal Mukami Kimathi Jumamosi, Mei 13 katika eneo la Njabini, Kinangop.

Maina Njenga
Maina Njenga
Image: STAR

Aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Maina Njenga siku ya Ijumaa alidai kuwa vikosi vya polisi vilivamia nyumba zake za Nairobi na Nyandarua kwa sababu zisizoeleweka.

Njenga alisema vikosi hivyo, ambavyo vilifika kwa wakati mmoja muda wa saa nne asubuhi katika nyumba zake za Lavington, Karen na Nyandarua, viliwaambia wafanyakazi wake kuwa walikuwa wakimtafuta.

Alisema kwa simu kuwa maafisa hao walibisha nyumbani kwake na kuruhusiwa kuingia kabla ya kuwachukua wafanyikazi kadhaa waliokuwa nyumbani kwake Lavington.

“Walisema wananitafuta. Sijui kwanini lakini naona ni siasa na unyanyasaji, jambo ambalo linapaswa kukomeshwa,” Njenga alisema.

Alihusisha uvamizi huo na ibada ya mazishi iliyopangwa ya mke wa Dedan Kimathi, Field Marshal Mukami Kimathi Jumamosi, Mei 13 katika eneo la Njabini, Kinangop.

Hakukuwa na majibu ya haraka kutoka kwa makao makuu ya polisi kuhusu madai hayo.

Njenga alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kumzuia kuhudhuria mazishi.

“Nilikuwa nyumbani kwa Kimathi siku ya Alhamisi na nikaambia familia tutakuja na baba (Raila) na nadhani hii ndiyo sababu wanafanya hivi. Ni mazishi na iwe hivyo,” aliongeza.

Alisema alikuwa mafichoni na kuomba unyanyasaji huo ukome na wafanyakazi wake waachiliwe.

“Wamefanya nini? Nimefanya nini? Poilisi wanaweza kunitumia wito wakinitaka lakini si kuvamia nyumba na kuwanyanyasa watu wasio na hatia.”

Alisema zama za kutumia polisi kuwanyanyasa wale wapinzani zilipitwa na wakati na kumtaka Rais William Ruto kuwadhibiti wale wanaofanya vitendo hivyo.

Rais Ruto ni miongoni mwa wanaotarajiwa katika mazishi ya serikali ya Mukami aliyefariki tarehe 4, Mei baada ya kuugua. Aliaga akiwa na umri wa miaka 96.

Kutakuwa na utazamaji wa hadharani wa mwili wa Mukami Jumamosi asubuhi kabla ya hafla ya mazishi ya umma itakayofanywa kwa heshima ya shujaa huyo wa kitaifa.