Ukiona kitu Raila anapinga jua ni kizuri - DP Gachagua kuhusu mswada wa fedha 2023

“Yule mtu ambaye anapinga huu mswa ni yule mzee wa Kitendawili. Yule wa kuvaa sufuria kwa kichwa. Na yeye anapinga kila kitu." - Gachagua.

Muhtasari

• Mbunge huyo wa zamani wa Mathira alisema kuwa mrengo wa upinzani ndio unapinga vikali mswada huo ukiongozwa na kinara wao Raila Odinga.

• Kulingana na Gachagua, kitu chochote ambacho Odinga anapinga basi hicho kinafaa kuchukuliwa kuwa sahihi.

DP Gachagua amuomba Odinga kusitisha maandamano.
DP Gachagua amuomba Odinga kusitisha maandamano.
Image: Facebook, Maktaba

Naibu wa rais Rigathi Gachagua amemhakikishia rais William Ruto kwamba wabunge wa eneo la Mlima Kenya na kila mtu wote wako nyuma ya mswada wa fedha wa 2023, huku mswada huo ukitarajiwa kuwasilishwa bungeni kujadiliwa kwa mara ya pili Alhamisi.

“Wajumbe wote katika Kenya Kwanza wako nyuma ya rais kwa mambo ya mswada wa fedha 2023. Wabunge wetu wote wako sawa na hapa katika hapa Mlima [Kenya] ni mia kwa mia, ni mmoja tu ndio anapiga kelele na ni sawa kwa sababu sisi ni watu wa demokrasia,” Gachagua alisema.

Mbunge huyo wa zamani wa Mathira alisema kuwa mrengo wa upinzani ndio unapinga vikali mswada huo ukiongozwa na kinara wao Raila Odinga.

Kulingana na Gachagua, kitu chochote ambacho Odinga anapinga basi hicho kinafaa kuchukuliwa kuwa sahihi.

“Yule mtu ambaye anapinga huu mswa ni yule mzee wa Kitendawili. Yule wa kuvaa sufuria kwa kichwa. Na yeye anapinga kila kitu. Ukiona kitu Raila anapinga ujue hicho kitu ni nzuri,” Gachagua alisema.

Gachagua alitolea mfano kaunti ya Kiambu akisema wabunge ni 12 lakini mmoja tu ndio anapinga na kusema kuwa huyo mmoja atanyamaza tu.

“Kiambu tuko na 12 lakini ni mmoja tu [akionyesha kwa ishara ya kidole cha shahada] ndio anapiga kelele, lakini atanyamaza,” alisema DP.

Kivangaito kinatarajiwa kushuhudiwa katika bunge la kitaifa baada ya mswada huo kuwasilishwa huku wabunge wanaoegemea upinzani wakiapa kuupinga vikali.

Mapema wiki hii, kinara wa Azimio Raila Odinga alisema kuwa mrengo huo ungetoa mwelekeo wao Alhamisi baada ya mswada huo kufikishwa bungeni.