Raila awaambia Wakenya kuwa tayari kwa ajili ya maandamano ya nchi nzima

Kiongozi huyo wa upinzani alisema atalihutubia taifa kuhusu Mswada tata wa Fedha wa 2023,

Muhtasari
  • Kiongozi huyo wa Azimio alisema miezi minane ya utawala wa Kenya Kwanza, Wakenya waliteseka zaidi kuliko hapo awali chini ya tawala zilizopita na kwamba sasa wamechoka.
KINARA WA MUUNGANO WA AZIMIO RAILA ODINGA
Image: TWITTER

Kiongozi wa muungano wa upinzani Azimio La Umoja Raila Odinga amewataka wakenya kuwa tayari kwa maandamano ya nchi nzima iwapo serikali haitatii wito wa kupunguza gharama ya maisha.

Akizungumza katika Chungwa House siku ya Jumatano alipokutana na wanachama wa Jumuiya ya Gusii wanaoishi Nairobi, Bw. Odinga alisema utawala unaoongozwa na Rais William Ruto ulikuwa ukiziba masikio yake kwa Wakenya wakiwemo wale wanaojiita wapiga kelele waliowaunga mkono katika uchaguzi uliopita.

Anasema utawala wa Kenya Kwanza umewapa mamilioni ya Wakenya masikio kiziwi kuhusu maswala kadhaa wanayoibua kuhusu gharama ya juu ya maisha na badala yake ilikuwa na mwelekeo wa kuwawekea utaratibu wa kutoza ushuru usiovumilika.

"Uongozi wa Kenya Kwanza umekataa kusikiliza kilio cha waendesha bodaboda, mama mboga,  na Wakenya wengine ambao hawawezi kumudu milo miwili kwa siku na wanasisitiza kutoza ushuru zaidi kwa watu ambao tayari wanateseka," alisema Odinga.

Kiongozi huyo wa upinzani alisema atalihutubia taifa kuhusu Mswada tata wa Fedha wa 2023, pamoja na wenzake katika Muungano wa Azimio La Umoja, na "atapiga tarumbeta" ili kuwapa Wakenya njia ya kusonga mbele.

"Wanataka kuwasilisha mswada tata bungeni kesho kwa kusomwa mara ya pili na kisha Waziri wa Hazina awasilishe taarifa ya bajeti Alhamisi wiki ijayo. Wamedhamiria kuipitisha, lakini Wakenya watapinga,” alisema.

Kiongozi huyo wa Azimio alisema miezi minane ya utawala wa Kenya Kwanza, Wakenya waliteseka zaidi kuliko hapo awali chini ya tawala zilizopita na kwamba sasa wamechoka.

“Wakenya wanaumia. Wanateseka. Waliingia mamlakani kupitia mlango wa nyuma wakati hawakuwa tayari kutawala na sasa wanataka kumwaga uzembe wao kwa Wakenya maskini”, alisema.