Hakuna mwanafunzi atatumwa nyumbani kwa kutolipa karo nitakapokuwa waziri wa elimu- Babu Owino

Mbunge huyo amedokeza matamanio yake ya kuchukua wadhifa wa waziri wa elimu katika siku za usoni.

Muhtasari

•Babu alisema moja ya malengo yake makuu atakapokuwa waziri ni kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi ambaye masomo yake yatakatizwa kwa kukosa karo.

•Hapo awali mbunge huyo amewahi kudai kuwa kufikia sasa amesoma na kupata  shahada tatu pamoja na Diploma tano.

Mbunge wa Embakasi East Babu Owino
Image: Facebook// Babu Owino

Mbunge mteule wa Embu Mashariki Paul Ongili almaarufu Babu Owino amedokeza matamanio yake ya kuchukua wadhifa wa waziri wa elimu katika siku za usoni.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, mwanasiasa huyo asiyepungukiwa na utata alisema moja ya malengo yake makuu atakapokuwa waziri ni kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi ambaye masomo yake yatakatizwa kwa kukosa karo.

"Nitakapokuwa waziri wa elimu nitahakikisha HAKUNA mwanafunzi anayerudishwa nyumbani kuendea karo ya shule," Babu Owino alisema.

Babu anatambulika kuwa mmoja wa wanasiasa vijana waliosoma zaidi nchini. Siku za hapo nyuma amewahi kujigamba kuhusu kufanya kozi nane katika chuo kikuu.

Hapo awali mbunge huyo amewahi kudai kuwa kufikia sasa amesoma na kupata  shahada tatu pamoja na Diploma tano.

"Mwana wenu wa kweli na kipenzi chenu Mhe.Babu Owino Paul Ongili Actuary-Actuarial Science First Class Honours ,Wakili-Second Class Upper,Masters In Actuarial science, Diploma katika Statistics, Diploma katika Ufundi, Diploma katika AstroPhysics, Diploma katika Ekonomia  na Diploma katika Industrial Chem." Alisema katika chapisho la awali.

Siku chache zilizopita, waziri wa elimu wa sasa George Magoha alitoa onyo kwa walimu wakuu dhidi ya kuwafukuza wanafunzi shuleni kwa kukosa karo.

Akizungumza Jumamosi mjini Mombasa, Magoha alisema hakuna mwalimu mwenye haki ya kurudisha mtoto nyumbani na akaahidi hatua kali za kinidhamu kutoka kwa wizara kwa wale ambao watakaidi agizo hilo.

"Uchumi ni mgumu sana kwa wazazi. Wazazi wengi wanatatizika na hivyo msimtume mtoto nyumbani kati ya sasa na mwisho wa mwaka. Mkifanya hivyo tutachukua hatua," Magoha alionya.

Magoha alisema kuwa mwalimu wa shule ya upili kutoka Shule ya Sekondari ya Matiku kaunti ya Makueni ambaye alikuwa amemrudisha mwanafunzi nyumbani ataadhibiwa na Tume ya Huduma ya Walimu.

Alisema mwalimu huyo alimtuma mwanafunzi huyo nyumbani kuchukua Sh1, 000 za masomo ya ziada.

“Huo ni wizi na lazima ukomeshwe, nakuhakikishia mwalimu ataadhibiwa,” alisema.