Maraga amkosoa rais Kenyatta

Jaji mkuu David Maraga. (Picha: HISANI )
Jaji mkuu David Maraga. (Picha: HISANI )

Jaji mkuu David Maraga amemkosoa rais Uhuru Kenyatta kwa kukataa kuwaapisha majaji 41 kama alivyoagizwa na mahakama.

Maraga ambaye anastaafu January 12 mwaka ujao, alisema kwamba rais anastahili kuwapisha  majaji hao ili kurahisisha utendakazi wa idara ya mahakama.

Jaji mkuu aliyasema haya  siku ya Ijumaa katika hafla ya uzinduzi wa ripoti ya hali ya idara ya mahakama. Hii ilikuwa hafla yake ya mwisho kama jaji mkuu kabla ya kustaafu.

Maraga alisema kwamba ameweza kuafikia mengi akiwa kiongozi wa idara ya mahakama licha ya mazingira magumu ya utendakazi kama vile muingilio na kuhujumiwa kwa wa idara hiyo pamoja na kupuuzwa kwa maagizo ya mahakama.

Alisema kwamba baada ya mahakama ya upeo kufutilia mbali uchaguzi wa urais mwaka 2017, Uhuru aliapa kuikabili idara hiyo na ametimiza ahadi hiyo kwani bajeti ya mahakama ilipunguzwa kwa kiasi kikubwa mwaka 2018.  

Kulingana na jaji mkuu ni miujiza kwamba wameweza kuwapa wakenya haki chini ya mazingira hayo magumu.

Aliwapongeza majaji na mahakimu kwa kupunguza mrundiko wa kesi na kuapa kwamba wataweza kumaliza kesi zote zilizokuwa zimekaa kwa muda mrefu, katika kipindi cha miaka miwili ijayo.  

"Licha ya changamoto hizi naomba majaji na mahakimu kuendelea kuwapa wakenya haki. Najivunia bidii yenu na mkumbuke kwamba idara ya mahakama inajukumu muhimu sana katika ustawi wa kisiasa nchini”.

"Ninapo ng’atuka katika muda wa siku chache zijazo nataka kuwahakikishia wakenya kwamba naacha idara thabiti ya mahakama. Idara ya mahakama inafaa kutengewa angalau asilimia tatu ya bajeti ya kitaifa,” jaji mkuu alisema.

Mgao wa kila mwaka wa miradi ya muundo msingi katika idara hiyo unafaa kuwa kati ya shilingi bilioni 5 na 10, alisema.

Maraga alisema kwamba hakuna uhasama kati yake na rais - "ni tofauti tu za kisera."

Aliongeza: "...ni wazi kwamba kuna tofauti za kisera kati yetu lakini nataka kukuhakikishia wewe (rais) sina kinyongo nawe".