COVID-19; mtoto azaliwa na kingamwili dhidi ya virusi

Muhtasari

• Mamake alikuwa na dalili wastani za Covid-19 akiwa mja mzito.

• Alilazwa kwa majuma mawili hospitalini kabla ya kurejea nyumbani.

• Madaktari wanachunguza uwezekano wa mama kumwambukiza mtoto akiwa tumboni 

Mama mmoja nchini Singapore aliyeambukizwa virusi vya Covid-19 mwezi Machi akiwa na mimba, amejifungua mtoto mwenye kingamwili dhidi ya Covid-19, na kuonyesha ishara kwamba kuna uwezekano maambukizi hayo yakasambazwa kutoka kwa mama hadi kwa  mtoto akiwa tumboni.

Mtoto huyo alizaliwa mwezi huu bila COVID-19 lakini akiwa na kingamwili dhidi ya virusi hivyo, jarida la Straits Times liliripoti siku ya Jumapili likimnukuu mamake.

“Madaktari wangu walishuku kwamba nilimpa kingamwili zangu dhidi ya covid-19 mwanangu wakati nilipokuwa mjamzito,” Celine Ng-Chan aliambia jarida hilo.

Ng-Chan alikuwa na dalili wastani za virusi hivyo na aliruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kulazwa kwa majuma mawili na nusu, jarida la Straits Times lilisema.

Shirika la afya duniani (WHO) limesema kwamba bado haijabainika ikiwa mwanamke mjamzito anaweza kumwambukiza mwanawe virusi akiwa tumboni au wakati wa kujifungua.

Kufikia sasa virusi hivyo havijapatikana katika sampuli za maji maji karibu na nyumba ,ya mtoto au katika maziwa ya mama.