Vijitabu vya kutia saini mswada wa BBI viko maeneo yote ya nchi

Rais Uhuru Kenyatta atia saini wakati wa hafla ya kuzindua saini za kufanikisha ripoti ya BBI. (Picha PSU)
Rais Uhuru Kenyatta atia saini wakati wa hafla ya kuzindua saini za kufanikisha ripoti ya BBI. (Picha PSU)

Click here to edit this text.

Vijitabu vya kutia sani ripoti ya BBI vimetumwa katika maeneo yote ya nchi, kulingana na mwenyekiti mwenza wa jopo linaloongoza shughuli hiyo Dennis Waweru.

Mbunge huyo wa zamani wa Dagoret South alitoa wito kwa wakenya kutembelea vituo vya ukusanyaji saini vilivyoko karibu nao kutia saini zao.

“Zoezi hilo lilianza vyema na kila eneo la nchi limepokea vijitabu. Tunahimiza wakenya wote kujitokeza kwa wingi kutia saini zao,” Waweru aliambia meza yetu ya habari kwa njia ya simu siku ya Ijumaa.

Waweru alisema zoezi la utiaji saini kupitia mfumo wa mtandaoni linaendelea vyema na alikuwa na matumaini  kwamba watapitisha saini milioni moja zinazohitajika kisheria.

Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga walizindia zoezi la ukusanyaji saini siku ya Jumatano. Saini hizo milioni moja ni za kufanikisha mageuzi ya katiba.

Kamati inayoongozwa na waweru na mbunge wa Suna East Junet Mohamed ina hadi Jumatano wiki ijayo kukamilisha zoezi hili.

Kulingana na ratiba yao, kamati ya Waweru na Junet inapaswa kuwasilisha saini hizo kwa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) Disemba 9 ili zikaguliwe.

Kulingana na katiba ikiwa IIEBC itaridhika na saini hizo, basi itawasilisha mswada huo kwa mabunge yote ya kaunti ili yaupige msasa na kisha kuidhinisha au kuukataa katika kipindi cha miezi mitatu.

Ikiwa mswada huo utapitishwa na angalau mabunge ya kaunti 24 kati ya 47 basi utawasilishwa moja kwa moja bungeni.

Kulingana na sheria,mswada huo utapita ikiwa utapata uungwaji mkono na wabunge wengi katika bunge la kitaifa na seneti na kisha kuidhinishwa na rais.

Hata hivyo kwa sababu mswada huu wa marekebisho unagusia nguzo muhimu za katiba ya 2010 na pia unalenga kufanyia mabadiliko bunge na ugatuzi lazima upelekwe kwa kura ya maamuzi.