Wakenya wakamatwa kwa kufanya 'ukahaba' nchini Bahrain

Muhtasari

• Ubalozi wa Kenya hupokea ripoti za kila siku kuhusu wakenya wanaokamatwa kwa makosa mbali mbali.

•Wengi wameshikwa kwa makosa ya ukahaba kuendesha masaji na kuuza pombe kinyume na sheria.

Makahaba (Picha; Maktaba)
Makahaba (Picha; Maktaba)

 Ubalozi wa Kenya nchini Bahrain umetowa tahadhari kwa wakenya wanaoishi nchini Bahrain dhidi ya kujihusisha na shughuli zinazokinzana na sheria za nchi hiyo.

Katika barua iliyotiwa saini na afisa mkuu wa ubalozi wa Kenya nchini Bahrain Raphael Musyoka, idadi ya wakenya wanaokamatwa nchini Bahrain kwa kuvunja sheria imeongezeka sana huku wengi wao wakizuiliwa korokoroni kwa sababu ya makosa mbali mbali.

Ubalonzi wa Kenya unasema kwamba kila siku wao hupokea ripoti ya wakenya waliotiwa mbaroni.

Kulingana na ubalozi huo wengi wa wakenya wameshikwa na hata kuhukumiwa huku wengine wakirejeshwa nchini kwa makosa ya kufanya ukahaba, kuuza pombe kinyume na sheria, ulevi na kusumbua umma, ukosefu wa stakabadhi za uhamiaji, kupata mimba haramu, kubadilisha ajira bila kuzingatia sheria za leba nchini humo, kuendesha shughuli za masaji na kuandaa hafla za nyumbani kinyume na sheria za nchi hiyo.

Ubalozi wa Kenya umetowa tahadhari kwa raia wake kuzingatia sheria za nchi hiyo ili kujiepusha na masaibu ya kukamatwa katika nchi ya kigeni.

Bahrain ni moja wapo ya nchi za kiarabu ambazo kuna idadi kubwa ya wakenya wanaofanya kazi hasa za mikono. Wengi wao wanafanya kazi za nyumbani, ulinzi, katika mahoteli, madereva na nyinine nyingi.