'Ruto' asajili chama kipya, wagombeaji wakabidhiwa vyeti

Makao makuu ya chama cha UDA mtaani Kilimani
Makao makuu ya chama cha UDA mtaani Kilimani
Image: Ezekiel Aminga

Chama United Democratic Alliance – kinachohuisishwa na naibu rais Willaim Ruto kimesajiliwa rasmi.

Hii ni ishara  tosha kwamba Ruto anaweka mikakati akijiandaa kukihama chama tawala cha Jubilee kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Msajili mkuu wa vyama vya kisiasa Anne Nderitu alithibitisha kubadilishwa kwa jina la chama cha Party of Development and Reform (PDR) hadi UDA. 

"Msajili wa vyama vya kisiasa anazingatia uamuzi uliochukuliwa na chama chako na mabadiliko yaliyotekelezwa Januari 7, 2021 baada ya kumalizika kwa kipindi kilichokubaliwa kisheria kulingana na Sehemu ya 20 (3A) ya PPA," Nderitu alisema.

Katika barua kwa katibu mkuu wa PDR, Nderitu alisema kuwa ofisi yake ilipokea mawasilisho kutoka kwa Khalid Njiraini Tianga ambaye alipinga utumiaji wa UDA lakini baadaye akaondoa malalamishi yake.

UDA siku ya Ijumaa kiliwapokeza wagombeaji kadhaa vyeti vya kushiriki chaguzi ndogo mbali mbali nchini ukiwemo uchaguzi wa gavana wa Nairobi.

Aliyekuwa mbunge wa Starehe Margaret Wanjiru amekabidhiwa cheti cha kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mdogo wa Nairobi. Uchaguzi huo hata hivyo umesimamishwa na mahakama kufutaia kesi iliyowasilishwa na aliyekuwa gavana Mike Sonko.

PDR ilikuwa imetoa ilani ya umma ya nia ya kubadilisha jina lake kuwa UDA na ishara yake kuwa toroli (wheelbarrow)  - kauli mbiu ya wafuasi wa Ruto.

Baada ya kupata idhini ya msajili wa vyama, UDA ilianzisha kampeni kali ya kuweka upya alama ikiwa ni pamoja na kupata ofisi kubwa ‘Hustler Centre’ katika mtaa wa Kilimani mjini.

Washirika wa Ruto walionyesha kufurahishwa na mabadiliko ya jina kwa mafanikio na kusambaza picha za makao yao mapya.

"Sasa ni rasmi, mtoto mpya mjini ni UDA zamani PDR ambaye alizaliwa mara ya pili," Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen alitweet.

Wachanganuzi walisema kwamba inaonekana kwamba washauri wa Naibu Rais walitaka kukwepa adhabu ya masharti ya kisheria yanayowazuia kujihusisha na chama kingine cha kisiasa kwa kupata PDR ambacho kina mkataba wa ushirikiano na muungano na Jubilee.