Magufuli: marehemu rais kuzikwa Alhamisi Machi, 25

Muhtasari

• Rais mpya wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alitangaza kwamba marehemu Magufuli atazikwa siku ya Alhamisi, Machi 25,2021 nyumbani kwake eneo la Chato.

Marehemu rais John Pombe Magufuli
Marehemu rais John Pombe Magufuli

 Mipango ya mazishi ya marehemu John Pombe Magufuli ambaye kufikia kifo chake alikuwa rais wa Tanzania imetangazwa.

Rais mpya wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alitangaza kwamba marehemu Magufuli atazikwa siku ya Alhamisi, Machi 25,2021 nyumbani kwake eneo la Chato.

Rais Samia Suluhu alitangaza kuwa wananchi watakuwa na fursa ya kuutazama mwili wake Magufuli ili kumpa marehemu rais heshima ya mwisho kuanzia Jumamosi, Machi 20.

Mwili utapelekwa katika uwanja wa Uhuru mjini Dar Es Salaam siku ya Jumamosi baada ya maombi.

Mwili wa marehumu rais Magufuli umehifadhiwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya kijeshi ya Lugalo.

Kulingana na ratiba iliyotangazwa na serikali ya Tanzania, mwili wa mwendazake utapelekwa katika mji mkuu wa Tanzania Dodoma Machi 21 ambapo marehemu atalala katika ikulu hadi siku itakayofuata na kisha kusafirishwa hadi mjini Mwanza.

Machi 23 mwili wa marehemu rais Magufuli utasafirishwa hadi nyumbani kwake eneo la Chato. Wenyeji wa Chato watapata fursa kuutazama mwili wa rais wao mnamo Machi 24.

Misa ya wafu ya mwendazake itafanyika katika kanisa katoliki la Chato Machi 25 na mazishi kufanyika siku iyo hiyo.

Marehemu Magufuli alizaliwa mwaka 1959 na alikuwa katika muhula wake wa pili kama rais wa Tanzania muhula ambao ulikuwa ukamilike mwaka 2025.

Tayari aliyekuwa makamu wake wa rais Samia Suluhu Hassan ameapishwa kuwa rais kukamilisha kipindi kilichokuwa kimesalia.