15 wafariki katika ajali kwenye barabara kuu ya Malindi - Mombasa

Muhtasari

• Kamishna wa kaunti ya Kilifi Kutswa Olaka alithibitisha ajali hiyo na kusema kwamba watu wasiopungua 14 walijeruhiwa katika ajali hiyo.

• Walioshuhudia ajali hiyo walisema basi la kampuni ya Muhsin kuelekea Garissa lilikuwa likijaribu kupita gari lingine na likapoteza mwelekeo  kabla kuogonga basi la Sabaki Shuttle.

Image: ALPHONSE GARI

Zaidi ya watu 15 wamefariki katika ajali mbaya ya barabarani iliohusisha mabasi mawili yaliogongana kwenye barabara kuu ya Malindi-Mombasa mapema siku ya Jumatano.

Kamishna wa kaunti ya Kilifi Kutswa Olaka alithibitisha ajali hiyo na kusema kwamba watu wasiopungua 14 walijeruhiwa katika ajali hiyo.

Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Kwamkikuyu na ilihusisha basi la kampuni ya Muhsin Bus lililokuwa safarini kwenda Garissa kutoka Mombasa na basi la kampuni ya Sabaki Shuttle lililokuwa likitoka Mombasa kwenda eneo la Merereni.

Madereva wote wawili walifariki papo hapo na kunahabari kwamba wafanyikazi kadha wa kaunti ya kilifi walihusika katika ajali hiyo.

Walioshuhudia ajali hiyo walisema basi la kampuni ya Muhsin kuelekea Garissa lilikuwa likijaribu kupita gari lingine na likapoteza mwelekeo  kabla kuogonga basi la Sabaki Shuttle.