Kondakta anusuru msichana kutoka kwenye mtego wa mnyanyasaji wa ngono

Msichana huyo mwenye umri wa ujana alikuwa ametongozwa kuenda Mariakani na mwanaume alikuja kumjua kupitia mtandao wa Facebook.

Muhtasari

•Msichana huyo ambaye alikamilisha masomo ya shule ya upili mwaka huu alidanganya kondakta wa basi hilo kuwa alikuwa anaenda kumwona kakake anayeishi Mariakani.

•Msichana huyo kumuona aliyekuja kumchukua alisema kuwa hawafanani kabisa na jamaa aliyekuwa anazungumza naye Facebook.

Machakos Country Bus
Machakos Country Bus
Image: The Star

Msichana mmoja kutoka kaunti ya Machakos aliponea chupu chupu kuanguka ndani ya mtego wa mnyanyasaji wa ngono.

Msichana huyo mwenye umri wa ujana alikuwa ametongozwa na mwanaume mmoja mkazi wa Pwani kupitia mtandao wa Facebook.

Bila ya kufahamu hatari iliyokuwa mbele yake, msichana huyo aliabiri basi la kampuni ya Executive katika kituo cha Machakos Junction na kufunga safari ya kuelekea Mombasa kama alivyokuwa ameagizwa na mnyanyasaji yule.

Msichana huyo ambaye alikamilisha masomo ya shule ya upili mwaka huu alidanganya kondakta wa basi hilo kuwa alikuwa anaenda kumwona kakake anayeishi Mariakani.

Kondakta alimuagiza msichana yule kulipa nauli ya Sh 1500 ila mfukoni alikuwa na Sh500 tu.Hapo kondakta akaamua kumpigia aliyedaiwa kuwa kaka ya msichana huyo simu ili asaidie kulipa nauli.

'Kaka' huyo aliahidi kuwa angelipa kabla ya basi kufika Mtito Andei ila ahadi ile haikutimizwa.

Hisia za shaka kuhusiana na aliyedaiwa kuwa kaka ya msichana huyo zilianza kumuingia kondakta walipokuwa wanaendelea na safari na walipofika Samburu akaamua kumdanganya jamaa huyo kuwa basi lilikuwa limefika Mariakani.

Mwanaume huyo alipoagizwa kufika kituoni kumchukua msichana aliambia kondakta amtumane kwa pikipiki hadi Kaloleni mahala ambapo wangepatana kisha alipe deni ya nauli.Kwa kuhofia usalama wa msichana yule, kondakta aliamua kuenda na abiria huyo hadi Mombasa.

Mhubiri aliyekuwa ameketi kando ya msichana huyo alimsihi msichana kumwambia kweli kuhusiana na jamaa yule.

Hapo ndipo msichana alifungua roho na kueleza kuwa yule hakuwa kakake ila ni mtu tu mgeni ambaye alimjua kupitia mtandao wa Facebook.

Basi lilipofika Mombasa mida ya saa kumi na nusu jioni, jamaa huyo hakuja kumchukua msichana hadi ilipofika saa mbili usiku.

Msichana huyo kumuona aliyekuja kumchukua alisema kuwa hawafanani kabisa na jamaa aliyekuwa anazungumza naye Facebook.

Baada ya tukio hilo la kuogofya msichana huyo alipewa mahali pa kulala na kurudishwa Machakos siku iliyofuata.

Kondakta aliyeokoa maisha yake alieleza kuwa kesi kama zile zilikuwa kwa wingi huku akitoa mfano wa msichana wa miaka 17 aliyepanda basi kuenda Mombasa kumuona mwanaume asiyemfahamu punde baada ya kumaliza mtihani wa KCSE.

Idara ya DCI imeripoti kuwa wanyanyasaji wa ngono wanatumia mitandao ya kijamii kuwafikia wasichana ambao wamemaliza masomo ya shule ya upili hivi majuzi na kuwateka nyara.

Kupitia mtandao wa Twitter, idara hiyo imesema kuwa waharifu hao wanatumia mitandao kupata habari za kibinafsi kuhusiana na wasichana hao kabla ya kuwadanganya kuingia kwenye mtego wao.

Maafisa wa polisi bado wanamuwinda mshukiwa huyo .

Wazazi wameagizwa kufuatilia shughuli za watoto wao mitandaoni na watu ambao wanazungumza nao kwa kuwa kesi za wasichana wadogo kutekwa nyara na kunyanyaswa kimapenzi zimepanda.