Kenya yapokea msaada wa dozi 358,700 za chanjo ya AstraZeneca kutoka Denmark

Hii inafuatia malalamishi ya upungufu wa dozi hizo haswa kutoka kwa wahudumu wa afya.

Muhtasari

•Chanjo hizo ambazo ni msaada kutoka taifa la Denmark ziliwasili  katika uwanja wa  ndege wa Jomo Kenyatta usiku wa Jumatatu na kupokelewa na maafisa katika wizara ya afya.

•Mochache alitangaza kuwa serikali ya Kenya inapanga kununua dozi milioni kumi za chanjo aina ya Johnson & Johnson ambazo zinatarajiwa kufika mwezi wa Agosti.

PS Susan Mochache akizungumza baada ya kupokea dozi za chanjo ya Korona usiku wa Jumatatu
PS Susan Mochache akizungumza baada ya kupokea dozi za chanjo ya Korona usiku wa Jumatatu
Image: Hisani

Kenya imepokea dozi 358, 700 za chanjo aina ya AstraZeneca kusaidia katika vita dhidi ya virusi vya Korona.

Chanjo hizo ambazo ni msaada kutoka taifa la Denmark ziliwasili  katika uwanja wa  ndege wa Jomo Kenyatta usiku wa Jumatatu na kupokelewa na maafisa katika wizara ya afya.

Wengine ambao walikuwemo ni pamoja na katibu wa utawala wa wizara ya  mashauri ya kigeni Ababu Namwamba, balozi wa Denmark, Ole Thonke na mwakilishi wa UNICEF Maniza Zaman.

Hii inafuatia malalamishi ya upungufu wa dozi hizo haswa kutoka kwa wahudumu wa afya.

Akipokea dozi hizo, katibu wa kudumu katika wizara ya afya Susan  Mochache alisema kuwa watakaopewa kipaumbele katika kupokea chanjo hizo ni watu ambao wako katika hatari ya kuambukizwa virusi vya Korona, wahadumu wa afya na wale ambao hawajapokea dozi yao ya pili.

"Mwito wetu kwa Wakenya ni kama ulipata dozi ya kwanza, tunaomba mjitokeze  kuanzia siku ya Jumatano kupata dozi yenu ya pili" Mochache alisema.

Mochache alisema kuwa chanjo hizo zina uwezo wa kudumu kwa kipindi cha mwezi mmoja 

Mochache alitangaza kuwa serikali ya Kenya inapanga kununua dozi milioni kumi za chanjo aina ya Johnson & Johnson ambazo zinatarajiwa kufika mwezi wa Agosti.

Kufikia siku ya Jumatatu, watu 995,570 walikuwa wamepata angalau dozi moja ya chanjo huku 192,093 pekee miongoni mwao wakipokea dozi ya pili.