Rais Kenyatta, Ruto na Raila waongoza taifa kufariji waziri Amina baada ya kifo cha mumewe

Rais Kenyatta alimsifia marehemu kama mwanafamilia imara, mwanabiashara mwenye kipaji na ambaye alichangia pakubwa katika uendeleshaji wa nchi.

Muhtasari

•Rais Kenyatta alimsifia marehemu kama mwanafamilia imara, mwanabiashara mwenye kipaji na ambaye alichangia pakubwa kwenye uendeleshaji wa nchi.

•Naibu rais William Ruto alimtaja marehemu kama mwanabiashara mwenye kipawa na ambaye alisaidia watu kupitia uwajibikaji wa kijamii.

•Kinara wa ODM Raila Odinga aliombea familia ya waziri Amina nguvu ya kustahimili msiba huo.

amina mohammed
amina mohammed

Asubuhi ya Alhamisi taifa liliamkia habari za kusikitisha kuhusu kifo cha mume wa waziri wa michezo Amina Mohammed.

Bw Khalid Ahmed alifariki alipokuwa anapokea matibabu katika hospitali ya Karen baada ya kuugua kwa kipindi kifupi.

Wakenya wengi wakiongozwa na viongozi wakuu wameendelea kufariji familia ya waziri Amina. Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga ni baadhi ya viongozi ambao wametuma jumbe zao za  rambirambi.

Rais Kenyatta alimsifia marehemu kama mwanafamilia imara, mwanabiashara mwenye kipaji na ambaye alichangia pakubwa katika uendeleshaji wa nchi.

"Ni jambo la kusikitisha kuwa kifo kimepokonya taifa letu mwanabiashara mwenye kipaji ambaye mchango wake katika uendeleshaji wa nchi utakumbukwa sana" Rais alisema.

Naibu rais William Ruto alimtaja marehemu kama mwanabiashara mwenye kipawa na ambaye alisaidia watu kupitia uwajibikaji wa kijamii.

"Tunasikitishwa na kifo cha Khalid Ahmed, mumewa waziri wa michezo Ambassador Amina Mohammed. Alikuwa mwanabiashara mwenye kipawa na ambaye alisaidia watu kupitia uwajibikaji wa kijamii. Tunaomba Mungu aifariji familia na wapendwa wao katika wakati huu wa majonzi. Pumzika kwa amani, Ahmed" Ruto alisema.

Kinara wa ODM Raila Odinga aliombea familia ya waziri Amina nguvu ya kustahimili msiba huo.

"Waziri Amina Mohammed, tafadhali kubali rambirambi zangu na Mama Ida kufuatia kifo cha mume wako uliyempenda Khalid Ahmed. Naomba Mungu akupe nguvu ya kustahimili hayo. Poleni sana." Raila alisema

Khalid ambaye ni baba wa wawili hakuonekana sana hadharani kwani alishughulika sana na familia na uendeleshaji wa mabiashara ya familia.