Mkasa wa moto: shule ya upili ya Sigalame yafungwa

Muhtasari

• Hiki ni kisa cha tatu cha moto katika shule hiyo katika kipindi cha chini ya miezi miwili hali ambayo imezua taharuki miongoni mwa wazazi na wadau wa shule hiyo ya wavulana.

Image: TWITTER.COM/SIGALAMEALUMNI/STATUS

Shule ya upili ya Sigalame katika kaunti ya Busia imefungwa kwa muda usiojulikana kufauatia kisha cha moto cha hivi punde katika msururu wa visa kama hivyo katika shule hiyo.

Kulingana na ujumbe uliyotumiwa wazazi na usimamizi wa shule hiyo moto uliteketeza bweni la Lenana katika shule hiyo usiku wa kuamkia siku ya Jumatano.

Hiki ni kisa cha tatu cha moto katika shule hiyo katika kipindi cha chini ya miezi miwili hali ambayo imezua taharuki miongoni mwa wazazi na wadau wa shule hiyo ya wavulana.

Usimamizi wa shule hiyo ulisema kwamba jumla ya wanafunzi 137 waliathirika kutokana na kisa cha hivi punde ingawa hakuna mwanafunzi aliyejeruhiwa kutokana na kisa hicho.

“Habari za asubuhi wazazi. Tulifungua na kutulia vizuri. Walakini tunataka kutoa ripoti kwamba kulikuwa na kisa cha moto ulioteketeza nyumba ya Lenana. Hii imeathiri wavulana 137. Wavulana wetu wote wako salama. Shule imefungwa na wavulana wameachiliwa kwenda nyumbani. Mawasiliano zaidi ya kufuata,” ujumbe uliyotumiwa wazazi ulieleza.

Muungano wa waliokuwa wanafunzi wa shule hiyo kupitia mtandao wa Twitter ulielezea masikitiko makubwa kufuatia msururu wa visa vya moto katika shule hiyo, ambayo ni moja wapo wa shule bora katika kaunti ya Busia.