Mzozo wa kimapenzi yaishia kwenye mauti - Wangige

Muhtasari

• John Tagei, 34,  aliyekuwa ameenda kumtembelea mpenzi wake majira ya asubuhi alishambuliwa na mwanamume mwingine.

Crime scene
Crime scene

Maafisa wa DCI wakishirikiana na polisi wa kawaida wameanzisha msako kumtafuta mwanamume aliyemuua mwenzake kutokana na mzozo wa kimapenzi Alhamisi asubuhi katika eneo la Wangige.

Kulingana na idara ya DCI marehemu  John Tagei, 34, ambaye alikuwa ameenda kumtembelea mpenzi wake majira ya asubuhi alishambuliwa na mwanamume mwingine aliyekuwa mpenzi wa zamani wa mwanamke huyo Loice Kanini.

Inasemekana marehemu Tagei alifika nyumbani kwa Kanini muda mfupi baada ya mwanawe Kanini kwenda shuleni.

Muda mfupi baadaye Kanini aligundua kwamba mwanawe alikuwa amesahau funguo zake nyumbani.

“Baada ya muda, Kanini aligundua kuwa mtoto wake alikuwa ameacha funguo zake nyumbani. Alimfuata akimuacha Tagei ndani ya nyumba. Alipokuwa anarudi, alikutana na mpenzi wake wa zamani Joseph Macharia, 33, ambaye alitaka kujua kwanini  alikuwa amemkaribisha mwanamume mwingine nyumbani kwake,” taarifa ya DCI ilieleza.

Kilichofuata ni makabiliano ambayo yaligeuka kuwa mauti, yakimuacha Tagei na majeraha mabaya.

Alikimbizwa katika hospitali ya Wangige Level IV.

Hata hivyo hali yake ilizorota na akahamishiwa katika hospitali ya PCEA Thogoto. Kwa bahati mbaya, alizidiwa na kuaga dunia.

Mshukiwa alitoroka na kwenda mafichoni.