Covid 19: Sekta ya kibananfsi yaruhusiwa kuagiza chanjo

Muhtasari

• Chanjo ya Johnson & Johnson yatarajia nchini Ijumaa ijayo.

• Tayari, Shilingi milioni 240 zimelipwa kwa akaunti hiyo na kutumwa kwa kwa Jumuiya ya Afrika.

• Sekta ya kibinafsi kufikia sasa imetenga shilingi bilioni moja ikiwa ni maandalizi ya ununuzi wa chanjo za Covid-19.

Sekta ya kibinafsi sasa inaweza kuendelea na mchakato wa upatikanaji wa chanjo za Covid-19 baada ya utaratibu wa ushiriki kukamilika na akaunti kufunguliwa katika Benki Kuu ya Kenya kwa lengo hilo.

Tayari, Shilingi milioni 240 zimelipwa kwa akaunti hiyo na kutumwa kwa kwa Jumuiya ya Afrika.

Angalau dozi 240,000 za chanjo za Johnson & Johnson zinatarajiwa kuwasili nchini wiki ijayo.

Huu ndio mchakato wa mwisho katika majadiliano ambayo yamekuwa yakiendelea kati ya Muungano wa Sekta ya binafsi ya Kenya na serikali na kupelekea kufanikisha ununuzi wa chanjo za Johnson na Johnson.

Angalau kampuni 263 tayari zimesajiliwa na kutoa malipo yao kwa juhudi hii kulingana na data ya KEPSA.

Mpango huo uko wazi kwa kampuni zote za sekta ya binafsi.

Chanjo hizo zitatumika kuwachanja wafanyikazi katika sekta hiyo, familia zao, na wananchi wengine kupiga jeki juhudi za serikali.

"Sasa tuna muundo wa ushiriki wa sekta ya binafsi, akaunti yao katika Hazina imefunguliwa wanaweza sasa kuendelea kuweka pesa na mchakato wa kusambaza chanjo utaanza," Waziri Mutahi Kagwe alisema.

“Hakutakuwa na uuzaji wa chanjo, ushiriki wa sekta ya binafsi ni kupitia Wizara ya Afya. Wanataka tu kuunga mkono juhudi za serikali na ninataka kuuliza wale wengine ambao wangependa kufanya hivyo, ”ameongeza.

Sekta ya kibinafsi kufikia sasa imetenga shilingi bilioni moja ikiwa ni maandalizi ya ununuzi wa chanjo za Covid-19.

Fedha hizo zinapaswa kuwekwa kwenye akaunti iliyofunguliwa na serikali itafanikisha ununuzi wa chanjo kwa kuwasilisha maombi ya ununuzi.

Chanjo hizo zitakapowasili nchini zitawekwa katika kituo maalum cha kuhifadhi chanjo eneo la Kitengela ambapo washiriki katika sekta ya binafsi watalazimika kupanga vile chanjo hizo zitatolewa kwa wanachama wake.

Afisa mkuu mtendaji wa KEPSA Carole Kariuki amebainisha kuwa sekta hiyo inashirikiana kwa karibu na wizara kujadili mpangilio wa maeneo yatakayo jumuishwa katika zoezi hilo.

"Serikali imekariri kuwa hakuna chanjo itakayouzwa nchini na KEPSA itazingatia maagizo haya kwa kutouza chanjo yoyote," Kariuki alisema.