Atwoli aagiza rais Kenyatta kuelezea kuhusu ongezeko la bei ya mafuta, atahadharisha serikali iwe tayari kwa migomo

Muhtasari

• Atwoli amesema kwamba hatua hiyo inakandamiza wafanyikazi nchini ambao tayari wanaumia kutokana na ushuru mkubwa na madhara ya janga la Corona.

•Atwoli ametahadharisha serikali iwe tayari kwa ghasia kubwa kutoka kwa sekta mbalimbali nchini iwapo hawataweka sera zake hazitaangazia wafanyikazi.

•Bosi huyo wa wafanyikazi nchini amemtaka rais Kenyatta kuhutubia wananchi kuhusiana na hatua kuongezewa kwa bei ya mafuta.

Katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli
Katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli

Katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli amelalamikia hatua ya serikali ya hivi karibuni kuongeza bei ya mafuta kwa shilingi saba.

Kupitia ujumbe uliotolewa kwa wanahabari siku ya Alhamisi, Atwoli amesema kwamba hatua hiyo inakandamiza wafanyikazi nchini ambao tayari wanaumia kutokana na ushuru mkubwa na madhara ya janga la Corona.

Atwoli ametahadharisha serikali iwe tayari kwa ghasia kubwa kutoka kwa sekta mbalimbali nchini iwapo hawataweka sera zake hazitaangazia wafanyikazi.

"Sisi kama COTU tunapinga kuongezewa kwa bei ya mafuta  na tunaagiza serikali kuwa bunifu kuhusu jinsi ya kupata ushuru. Kwa wakati huo huo tungependa kukumbusha rais kwamba wafanyikazi wanaumia na hafai kukubali kutojali, kuadhibiwa na kunyanyaswa kwa wafanyikazi wa Kenya na idara kama ya EPRA" Atwoli amesema.

Bosi huyo wa wafanyikazi nchini amemtaka rais Kenyatta kuhutubia wananchi kuhusiana na hatua kuongezewa kwa bei ya mafuta.

"Rais mwenyewe anafaa kueleza Wakenya mbona serikali iko makini sana kuongeza uchungu na maumivu ya wafanyikazi wa Kenya na Wakenya wote kwa jumla wakati bado kuna janga la Corona" Atwoli amesema.

Kulingana na Atwoli, inagharimu nchini shilingi 49.84 pekee kusafirisha lita moja ya petroli kutoka Middle East ilhali Wakenya wanalazimika kulipa shilingi 84 zaidi kwa kila lita moja ya petroli ambayo wananunua.