Mahakama yapata Itumbi na kesi ya kujibu kuhusiana na barua bandia iliyozungumzia njama ya kuua naibu rais

Muhtasari

•Hakimu mkuu Martha Mutuku wa mahakama ya Milimani alitoa aliagiza Itumbi pamoja na mshtakiwa mwenza Samuel Gateri wajitetee baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kesi dhidi yao

•Barua ambayo wawili hao walishtakiwa kuchapisha mwaka wa 2019  ilidai kwamba kulikuwa na mkutano ambao ulikuwa umepangwa kufanyika katika hoteli ya La Mada ili kujadili njama ya kuua naibu rais.

Image: EZEKIEL AMINGA

Mwandishi Dennis Itumbi ameagizwa kujitetea baada ya mahakama kuamuru kuwa ako na kesi ya kujibu kuhusiana na barua bandia iliyoeleza njama ya kuua naibu rais William Ruto.

Hakimu mkuu Martha Mutuku wa mahakama ya Milimani alitoa aliagiza Itumbi pamoja na mshtakiwa mwenza Samuel Gateri wajitetee baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kesi dhidi yao.

Mutuku alisema kuwa kesi hiyo itatajwa tena siku ya  Alhamisi ili tarehe  maalum ya kusikizwa kwa kesi hiyo itengwe.

Mwezi Agosti itumbi kupitia wakili wake Katwa Kigen alikuwa ameomba mahakama kutupilia mbali mashtaka ya kutengeneza na kuchapisha karatasi bandia  pamoja na uharibifu wa mitambo ya simu dhidi yake kwa ukosefu wa ushahidi.

Upande wa mashtaka uliita mashahidi wanane kuthibitisha kesi yao dhidi ya Itumbi na mwanablogu Samuel Gateri.

Barua ambayo wawili hao walishtakiwa kuchapisha mwaka wa 2019  ilidai kwamba kulikuwa na mkutano ambao ulikuwa umepangwa kufanyika katika hoteli ya La Mada ili kujadili njama ya kuua naibu rais.

Mahakama sasa inawataka Itumbi na Gateri kueleza kilichotokea.