Raila aahidi kutenga nafasi nne za uwaziri kwa vijana iwapo atachaguliwa kuwa rais

Muhtasari

•Raila ambaye ameongeza kasi katika safari ya kujipigia debe pia alisema kuwa serikali yake itahifadhi nafasi nyingi zaidi kwa vijana.

•Kiongozi huyo wa ODM aliahidi kuunda idara ya vijana kwenye wizara ya masuala ya kigeni kwani raia wengi ambao wanaishi nje ya nchi ni vijana.

•Raila alisema kuwa iwapo vijana watawezeshwa vizuri watakuwa chanzo cha utajiri nchini na kupunguza asilimia ya watu wasio na kazi.

Raila Odinga akiwa Homabay
Raila Odinga akiwa Homabay
Image: MARTIN OMBIMA

Kinara wa ODM Raila Odinga ameahidi kuteua angalau vijana wanne kwenye baraza la mawaziri iwapo atachaguliwa kuwa rais mwaka ujao.

Kiongozi huyo wa upinzani alitoa ahadi hiyo siku ya Jumanne alipokuwa amekutana na kikundi cha vijana kutoka eneo la Mlima Kenya katika jitihada za kushawishi vijana tunapokaribia chaguzi kuu za mwaka wa 2022.

Raila ambaye ameongeza kasi katika safari ya kujipigia debe pia alisema kuwa serikali yake itahifadhi nafasi nyingi zaidi kwa vijana.

Alisisitiza kuwa ataweka vijana moyoni iwapo atachaguliwa kuingia ikulu ili kuwawezesha.

"Katika suala la nafasi za uwaziri kwa vijana, zitakuwa zaidi ya nne"  Raila alisema.

Raila alisema kuwa alipokuwa waziri mkuu wakati wa serikali ya nusu mkate hakuangusha vijana.

"Nilipokuwa waziri mkuu, nilishiriki mikutano na jamii ya wafanyibiashara na vijana. Mikutano hiyo ilifanyika mara nne kila mwaka ili tupate kusikia changamoto ambazo vijana walikuwa wanapitia na tulichokuwa tunafanya. Ni kitu ambacho nimejaribu hapo awali na itakuwa moja ya sera zangu" Alisema Raila.

Aliomba vijana kuwa pamoja naye katika azimio lake la kuwa rais kwa kumpigia debe.

Kiongozi huyo wa ODM aliahidi kuunda idara ya vijana kwenye wizara ya masuala ya kigeni kwani raia wengi ambao wanaishi nje ya nchi ni vijana.

Kulingana na sensa ya 2019, vijana ni 75% ya watu milioni 47.6 walio nchini.

Takwimu hizi zimelazimu wagombeaji wa kiti cha urais kuunda sera ambazo zinapendelea vijana ili kuwafurahisha.

Raila alisema kuwa iwapo vijana watawezeshwa vizuri watakuwa chanzo cha utajiri nchini na kupunguza asilimia ya watu wasio na kazi.

"Usipoelimisha vijana na kuwapa ujuzi unaohitajika, watakuwa walanguzi wa madawa ya kulevya kwenye jamii lakini iwapo watawezeshwa watakuwa chanzo kizuri cha utajiri. Ndio maana tunafaa kuangazia suala hili sana" Raila alisema.

Raila pia alisema kuwa hatua inafaa kuchukuliwa ili kuongeza uwakilishaji wa wanawake uongozini.