Jamaa aliyejaribu kutenganisha vita kati ya wanaume wawili auawa kwa kisu Nyeri

Muhtasari

•Kulingana na DCI, mhasiriwa alianguka kwa kishindo huku damu ikibubujika shingoni alipoenda kujaribu kutenganisha wanaume wawili ambao walikuwa wanapimana nguvu kufuatia mzozo ambao haujathibitishwa.

•Uchunguzi zaidi wa polisi ulibaini kuwa mshukiwa alikuwa amemdunga mwenzake ambaye walihusika kwenye vita naye  tumboni kabla ya kumdunga marehemu kwenye shingo.

Crime scene
Crime scene

Jamaa mmoja aliyejaribu kutenganisha vita kati ya wanaume wawili alipoteza maisha yake baada ya mmoja wao kumdunga vibaya kwa kisu.

John Kagwe (26)  anaripotiwa kumdunga marehemu kwenye shingo kwa kutumia kisu ambacho alikuwa ameficha mwilini katika soko ya Kieni Barrier, kaunti ya Nyeri.

Kulingana na DCI, mhasiriwa alianguka kwa kishindo huku damu ikibubujika shingoni alipoenda kujaribu kutenganisha wanaume wawili ambao walikuwa wanapimana nguvu kufuatia mzozo ambao haujathibitishwa.

Wasamaria wema ambao walishuhudia tukio lile walimkimbiza mhasiriwa katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Nyeri wakikusudia kuokoa maisha yake ila akatangazwa kuwa maiti punde baada ya kufikishwa pale.

Uchunguzi zaidi wa polisi ulibaini kuwa mshukiwa alikuwa amemdunga mwenzake ambaye walihusika kwenye vita naye  tumboni kabla ya kumdunga marehemu kwenye shingo.

Kwa bahati nzuri mhasiriwa wa kwanza aliweza kutibiwa katika kituo cha afya kilichokuwa karibu na kupewa ruhusa kuenda nyumbani kwani jeraha lake halikuwa mbaya sana.

Mshukiwa alikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha Narumoru huku akisubiri kufikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa la mauaji.