Mike Sonko akubali kushindwa baada ya mahakama kuidhinisha kuapishwa kwa Anne Kananu

Muhtasari

•Sonko amesema uamuzi ambao mahakama kuu zaidi nchini iilitoa alasiri ya Jumatatu hautavunja moyo wake katika siasa huku akiashiria atarejea tena.

•Siku ya Jumatatu mahakamu kuu zaidi nchini ilitupilia mbali ombi la Mike Sonko la kuzuia  kuapishwa kwa Anne Kananu kama gavana mpya wa Nairobi.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Image: FACEBOOK// MIKE SONKO

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Gideon Kioko Mbuvi almaarufu kama Mike Sonko amekubali kushindwa katika kesi aliyokuwa amewasilisha mahakamani akipinga kuapishwa kazini kwa Anne Kananu.

Sonko alitumia kurasa zake za mitandao  ya kijamii kusema uamuzi ambao mahakama kuu zaidi nchini iilitoa alasiri ya Jumatatu hautavunja moyo wake katika siasa huku akiashiria atarejea tena.

Mwanasiasa huyo asiyepungukiwa na drama ametoa shukrani kwa nafasi aliyokuwa amepatiwa ingawa alipokonywa mnamo mwezi Desemba mwaka uliopita

"Wakenya wenzangu, nakubali kushindwa baada ya uamuzi wa mahakama kuu zaidi nchini alasiri ya leo (Jumatatu). Wakati wa Mungu ndio mzuri zaidi na wakati utakuja ambapo atanipatia nafasi nyingine ya kuhudumia Wakenya katika nafasi yoyote. Nashukuru kila wakati kwa nafasi ya kuwafanyia kazi, nitaendelea kufanya hivyo. Kwa sasa tuwache yote kwa Mungu. Tutajaribu wakati mwingine, alluta continua kwani maisha lazima yaendelee. Twendeni tupige sherehe sasa" Sonko alisema.

Siku ya Jumatatu mahakamu kuu zaidi nchini ilitupilia mbali ombi la Mike Sonko la kuzuia  kuapishwa kwa Anne Kananu kama gavana mpya wa Nairobi.

 Mnamo Oktoba 25 jaji Mohammed Ibrahim aliagiza kamati iliyokuwa inaendelea mchakato wa kukabidhi Kananu afisi ya gavana isimamishe kuapishwa kwake kwa wiki mbili ili kupatia nafasi kusikizwa kwa kesi ya Sonko.

Hata hivyo, rufaa kuu ambayo iliwasilishwa katika mahakama ya kukata rufaa bado halijasikizwa na kuamuliwa. Naibu msajili wa mahakama atatoa maelekezo zaidi kuhusu kesi huyo mnamo Novemba 15.