Mzee wa miaka 70 aliyedunga mkewe hadi kifo kufuatia mzozo wa Sh6000 akamatwa Embu

Muhtasari

•Alipohojiwa na chifu aliyemuokoa kutoka kwa umati uliotaka kumuadhibu, Njue alikiri kutenda unyama huo kutokana na hasira.

•Mshukiwa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Runyenjes huku mwili wa marehemu ukiwa umehifadhiwa katika mochari ya hospitali ya Embu Level 5

Luka Njue ambaye alidunga mke wake akiwa ndani ya gari ya polisi katika kijiji cha Thau, Embu siku ya Jumanne Novemba 9, 2021
Luka Njue ambaye alidunga mke wake akiwa ndani ya gari ya polisi katika kijiji cha Thau, Embu siku ya Jumanne Novemba 9, 2021
Image: BENJAMIN NYAGA

Polisi katika eneo la Runyenjes, kaunti ya Embu wamekamata mwanaume mwenye umri wa miaka 70 anayedaiwa kudunga mkewe wa miaka 46 hadi kifo.

Luka Njue anaripotiwa kuua mke wake Nancy Muthoni kwa kutumia kisu chenye makali alasiri ya Jumanne.

Majirani wenye ghadhabu ambao walifika kwenye eneo la tukio baada ya kusikia mayowe makali ya marehemu walishambulia mshukiwa kabla ya chifu wa eneo hilo Ndwiga Kagaari kuingilia kati na kumuokoa.

Alipohojiwa na chifu aliyemuokoa kutoka kwa umati uliotaka kumuadhibu, Njue alikiri kutenda unyama huo kutokana na hasira.

Alidai kwamba mkewe alikuwa ameiba pesa zake shilingi elfu ita ambazo alikuwa amepata baada ya kuuza mbuzi.

Chifu alisema kisu kilichotumika kutekeleza mauaji hayo kilipatikana.

Wabakijiji waliojitokeza kushuhudia tukio hilo katika kijiji cha Thau, Runyejes
Wabakijiji waliojitokeza kushuhudia tukio hilo katika kijiji cha Thau, Runyejes
Image: BENJAMIN NYAGA

Wanandoa hao wanadaiwa kuanza kulumbana mwendo wa saa saba mchana wakiwa nyuma ya baa moja katika eneo hilo.

Malumbano makali yalianza baada ya mshukiwa kuuliza marehemu mahali pesa zake zilikuwa zimeenda.

Kulingana na mzee mmoja wa kijiji anayejulikana kama Jeremiah Nthiga, familia hiyo imekuwa ikiishi kwa vurugu.

Alisema amekuwa akijaribu kuwaongelesha mara kwa mara na kusuluhisha mizozo mbalimbali.

Mshukiwa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Runyenjes huku mwili wa marehemu ukiwa umehifadhiwa katika mochari ya hospitali ya Embu Level 5.

(Utafsiri: Samuel Maina)