Uhuru aomboleza kifo cha mamake Tuju

Muhtasari

• Rais Uhuru Kenyatta ametuma rambirambi kwa familia ya Katibu Mkuu wa Jubilee na Waziri Raphael Tuju kufuatia kifo cha mama yao Mama Mary Odiyo Tuju. 

 

Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta ametuma rambirambi kwa familia ya Katibu Mkuu wa Jubilee na Waziri Raphael Tuju kufuatia kifo cha mama yao Mama Mary Odiyo Tuju. 

Mama Mary, 87, aliaga dunia usiku wa kuamkia Jumatano alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali moja ya Nairobi. Katika ujumbe wake wa kuifariji familia, Rais alimsifu Mama Mary kuwa kiongozi na mzee wa jamii mchapakazi ambaye alithamini na kuunga mkono kwa kiasi kikubwa elimu kama msingi wa maisha.

 “Mama Mary alikuwa kiongozi wa jamii anayejulikana na aliyeheshimika sana ambaye aliamini katika fadhila na manufaa ya elimu. Imani yake kwamba elimu ndio msingi wa maisha ndiyo msukumo uliowaongoza wengi kutoka kwa jamii yake kufuata elimu, na kuwa wanajamii wenye tija,” Rais alisema. 

Kiongozi huyo wa taifa alimuelezea Mama Mary kuwa ni mama imara aliyelea familia yenye mafanikio na kumuomba Mwenyezi Mungu aipe familia ya Tuju faraja na ujasiri katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

 "Tutamshukuru milele kwa kazi ambayo amefanya kwa taifa letu na kulea familia yenye nguvu ambayo imeendelea kuchangia mabadiliko ya kijamii na kiuchumi katika nchi yetu," Uhuru alisema. 

“Naomba Mungu azidi kumwaga upendo na amani yake mioyoni mwenu mnapoomboleza kifo cha mama yenu mpendwa. Ninakuhakikishia maombi yangu na uungwaji mkono unapokubali kifo cha mama wa familia yako,” Rais Kenyatta alifariji familia.