Maafisa 2 wa magereza kizimbani leo

Muhtasari

• Maafisa hao ni pamoja na anayesimamia Gereza la Kamiti ambapo wafungwa hao walitoroka.

• Maafisa  wengine walifikishwa kortini na mahakama ikaamuru wazuiliwe kwa siku 25 huku uchunguzi ukiendelea.

 

Aliyekuwa Mkuu wa magereza Wycliffe Ogalo atiwa mbaroni
Image: Laura Shatuma

Maafisa wawili zaidi wa magereza wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo asubuhi kutokana na kutoroka kwa wafungwa watatu waliokuwa wakitumikia kifungo kwa uhalifu unaohusiana na ugaidi.

Maafisa hao ni pamoja na anayesimamia Gereza la Kamiti ambapo wafungwa hao walitoroka. Hii itaongezeka hadi kumi, idadi ya maafisa walioko kizuizini kufikia sasa kuhusu kutoroka kwa Musharraf Abdalla Akhulunga a.k.a Zarkarawi, Mohammed Ali Abikar na Joseph Juma Odhiambo a.k.a Yusuf.

 Maafisa  wengine walifikishwa kortini na mahakama ikaamuru wazuiliwe kwa siku 25 huku uchunguzi ukiendelea.

Kamishna wa magereza Wycliffe Ogalo alifutwa kazi siku ya Jumatano kutokana na kisa hicho huku uchunguzi ukiendelea.

Kwingineko, Polisi huko Isiolo wanasaka genge lililojihami ambalo lilivamia baa moja eneo hilo, na kumpiga risasi mlinzi kwenye paja na kuwajeruhi wengine watano kabla ya kutoroka na kiasi cha pesa kisichojulikana Jumatano jioni. 

Mmoja wa washukiwa hao alipigwa risasi na kuuawa katika tukio wakati polisi walikuwa wakiwakabili.

Polisi wanasema washukiwa wengine watatu wenye silaha walifanikiwa kutoroka katika kisa hicho lakini juhudi za kuwapata zinaendelea.