Afisa wa kaunti ya Kisumu anayedaiwa kuongoza kundi lililovamia msafara wa Ruto ashtakiwa

Wilson Ajuang Aminda alishtakiwa kwa makosa mawili tofauti

Muhtasari

•Mshukiwa alikanusha mashtaka yote mawili dhidi yake na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi 500,000

Wilson Aminda katika mahakama ya Winam siku ya Alhamisi
Wilson Aminda katika mahakama ya Winam siku ya Alhamisi
Image: FAITH MATETE

Habari na Faith Matete

Mfanyikazi mmoja wa kaunti ya Kisumu ambaye alikamatwa siku ya Jumatatu baada ya kudaiwa kuongoza umati uliopiga msafara wa naibu rais kwa mawe wiki iliyopita alifikishwa mahakamani Alhamisi.

Wilson Ajuang Aminda alishtakiwa kwa makosa mawili tofauti mbele ya hakimu  mkuu mwandamizi Robert Wanda wa mahakama ya Winam

Kulingana na karatasi ya mashtaka, mshukiwa kwa ushirikiano na wengine ambao hawakufikishwa mahakamani waliharibu sehemu mbalimbali za magari matano ya serikali ya Kenya kwa makusudi na kinyume na sheria mnamo Novemba 10, 2021 katika mzunguko wa barabara wa Kondele, kaunti ndogo .

Aminda pia alishtakiwa kwa kusababisha usumbufu kwa namna ambayo inaweza kusababisha ukosefu wa amani, kinyume na sheria.

Mshukiwa hata hivyo alikanusha mashtaka yote mawili dhidi yake na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi 500,000 au mbadala wa shilingi 100,000 pesa taslimu.

Hakimu aliamuru kesi hiyo itajwe tena mnamo Februari 7, 2021.

Mnamo Novemba 10 wakati ambapo Ruto alikuwa katika ziara ya kampeni katika eneo la Nyanza, msafara wa magari yake ulishambuliwa kwa mawe na kikundi cha vijana na akalazimika kukatiza hotuba yake.

Polisi walijaribu kuthibiti tukio hilo kwa kutawanya umati kutumia gesi ya machozi.

Aminda alikamatwa siku ya Jumatatu baada ya kuhusishwa na mashambulio hayo.