Washukiwa wa mauaji ya wakongwe 4 Kisii kusalia rumande

Kesi ya mauaji itatajwa tena tarehe 15 Disemba 2021

Muhtasari

• Washukiwa sita wanaoshtakiwa kwa kuwateketeza wakongwe wanne katika Kaunti ya Kisii watazuiliwa korokoroni kwa muda wa wiki mbili zijazo.

• Jaji wa Mahakama Kuu mjini Kisii, Rose Ougo, aliamuru washtakiwa kusalia katika Gereza la Kisii GK wakisubiri uamuzi wa ombi la dhamana lililowasilishwa na wakili wao.  

• Kesi ya mauaji itatajwa tena tarehe 15 Disemba 2021.

Washukiwa sita wanaoshtakiwa kwa kuwateketeza wakongwe wanne kwa tuhuma za uchawi eneo la Marani, Kaunti ya Kisii watazuiliwa korokoroni kwa muda wa wiki mbili zijazo wakisubiri uamuzi wa ombi lao la kuachiliwa kwa dhamana.            

Wakili wa Serikali Susan Kibungi alipinga ombi la dhamana kwa madai kuwa kuna sababu za msingi za washtakiwa kutoachiliwa akisema wana uwezekano wa kuwaingilia mashahidi.

             Wakili huyo alisema kulikuwa na mvutano mkubwa chinichini na washtakiwa hawapaswi kupewa dhamana na kuongeza kuwa mengi yanaweza kutokea kwa kuwa usalama wao hauna hakikisho.            

Wakili John Khaminwa, ambaye aliwakilisha Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya kwa familia za waathiriwa pia alipinga ombi la dhamana akisema kuwa familia hizo zilikuwa zikipokea vitisho kutoka kwa washukiwa na maisha yao yalikuwa hatarini.            

Alifahamisha mahakama kuwa wapo watu wengine katika maeneo ya vijijini waliohusika katika mauaji ya wakongwe hao ambao hawajakamatwa na orodha hiyo ilipelekwa kwa mgurugenzi wa DCI.            

Wakili Khaminwa alisema kuwa kando na kosa hilo linalotekelezwa katika Kaunti ya Kisii, hali ni hiyo hiyo katika baadhi ya maeneo ya Pwani na baadhi ya maeneo ya Magharibi mwa Kenya akisema ni lazima hatua madhubuti zichukuliwe dhidi ya watuhumiwa ili liwe funzo kwa wengine.              

Wakili wa washitakiwa, Shaffin Kaba, alisema wateja wake hawana hatia hadi itakapothibitishwa na wana haki ya kupewa dhamana kwa kuwa hakuna sababu za msingi zilizotolewa na upande wa mashtaka kuwanyima haki ya dhamana.            

Kaba, aliiomba mahakama hiyo kupuuza taarifa ya afisa wa uangalizi iliyodai kwamba washukiwa walikiri kuua wakongwe hao.             Wakili huyo alidai kuwa washtakiwa hawajawatishia mashahidi wakiwa rumande kama ilivyosemwa na Wakili wa Serikali akidai.

Kaba aliiomba mahakama kuzingatia mambo ya msingi ya haki na kuweka uwiano kati ya kulinda uhuru wa mtu binafsi na kulinda utawala bora wa haki.            

Jaji wa Mahakama Kuu mjini Kisii, Rose Ougo, aliamuru washtakiwa kusalia katika Gereza la Kisii GK wakisubiri uamuzi wa ombi la dhamana lililowasilishwa na wakili wao.            

Washukiwa hao, Amos Nyakundi Ondieki, Chrispine Makworo Ogeto, Peter Angwenyi Gwanga, Brian Mecha Nyakundi, Ronald Ombati Onyonka na Justin Morara walikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji ya wakongwe wanne kwa tuhuma za uchawi katika eneo la Marani, Kaunti ya Kisii mnamo Oktoba 17, 2021. 

Kesi ya mauaji itatajwa tena tarehe 15 Disemba 2021.