'Boma moja, Ng'ombe mmoja!' Mwangi Wa Iria aahidi kupatia kila Mkenya ng’ombe akichaguliwa kuwa rais

Alisisitiza kwamba ana matumaini makubwa ya kuridhi kiti cha rais Uhuru Kenyatta

Muhtasari

•Alitoa wito kwa Wakenya walio na uwezo wa kifedha kumpatia ng'ombe ili aweze kusambaza kwa wengine wasio na uwezo mkubwa.

•Wa Iria alisema wagombeaji wa viti tofauti kitumia tikiti ya chama chake watahitajika kutoa idadi fulani ya ng'ombe kulingana na cheo cha kiti wanachomezea mate.

Gavana Mwangi Wa Iria akihutubia waandishi wa habari
Gavana Mwangi Wa Iria akihutubia waandishi wa habari
Image: BERNARD MUNYAO

Gavana wa Murang'a Mwangi Wa Iria ameapa kupatia kila mwananchi ng'ombe mmoja iwapo atachaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya Kenya katika chaguzi kuu za mwezi Agosti.

Alipokuwa anahutubia wanahabari siku ya Jumatano, Wa Iria alisisitiza kwamba ana matumaini makubwa ya kuridhi kiti cha rais Uhuru Kenyatta atakapostaafu takriban miezi 8 ijayo.

Gavana huyo alisema tofauti na wagombeaji wengine ambao wametoa ahadi za pesa watakapochaguliwa, serikali yake itahakikisha kwamba kila boma imepata angalau ng'ombe mmoja.

"Wengine wamesema watapeana elfu sita kwa wale hawana kazi. Mimi nikiwa rais wa Kenya, kwa sababu nitakuwa, kila mtu ambaye ni mkulima na hana ng'ombe serikali yangu itapeana ng'ombe kwa kila mwananchi. Boma moja, ng'ombe mmoja. Na nitaweka kwa sheria. Hiyo sheria nitaianza sasa hata kabla nichaguliwe"  Mwangi alisema.

Mgombeaji huyo wa kiti cha urais kwa tikiti ya chama cha Usawa Kwa Wote alitoa wito kwa Wakenya walio na uwezo wa kifedha kumpatia ng'ombe ili aweze kusambaza kwa wengine wasio na uwezo mkubwa.

Hali kadhalika aliongeza kuwa  wagombeaji wote ambao wanatazamia kuwania kwa tikiti ya chama chake watalazimika kutoa ng'ombe kadhaa kulingana na makubaliano yatakayoafikiwa na kamati yake  ili kukabidhiwa cheti.

"Ningewaomba Wakenya wapatie chama cha usawa ng'ombe ili tusambaze kwa Wakenya ambao hawana uwezo na hata walemavu. Katika chama changu sheria moja ni kwamba ili uwe mgombeaji lazima utoe ng'ombe. Nimeweka kwa sheria na imeidhinishwa na IEBC" Alisema Mwangi.

Wa Iria alisema wagombeaji wa viti tofauti kitumia tikiti ya chama chake watahitajika kutoa idadi fulani ya ng'ombe kulingana na cheo cha kiti wanachomezea mate.