Miguna Miguna amkosoa Ruto kwa kuomba msamaha kufuatia matamshi ya Linturi 'madoadoa'

Muhtasari

•Kulingana na Miguna, mateso ya seneta Linturi ni ya kisiasa na haikuwa na haja naibu rais William Ruto kuomba msamaha.

Image: TWITTER// MIGUNA MIGUNA

Wakili na mwanasiasa maarufu Miguna Miguna ametoa maoni yake kuhusiana na matamshi ya seneta wa Meru Mithika Linturi 'madoadoa' .

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Miguna amesema matamshi ya mwandani huyo wa naibu rais yalikuwa maoni yasiyohitaji udhibiti wa serikali na hayakumaanisha uhalifu.

Kulingana na Miguna, mateso ya seneta Linturi ni ya kisiasa na haikuwa na haja naibu rais William Ruto kuomba msamaha.

"Maoni ya Mithika Linturi ya "madoadoa" hayakuwa ya kihalifu na ni hotuba iliyolindwa. Mateso yake ni ya kisiasa. Hakuna sababu kabisa kwa nini @WilliamsRuto ameomba msamaha isipokuwa kwamba anathamini mamlaka juu ya kanuni" Miguna aliandika.

Wakili huyo ameagiza hatua sawa kuchukuliwa dhidi ya wachochezi wote bila ubaguzi wa aina yoyote kwa misingi ya kisiasa.

Miguna pia alihimiza Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga kupigania haki ya uchaguzi na kuhakikisha uchaguzi wa mwezi Agosti utakuwa huru, wa haki na wa kuaminika.

"DP William Ruto, Raila Odinga na wafuasi wao wanapaswa kupigania haki ya uchaguzi na kuhakikisha kwamba uchaguzi wa 2022 ni huru, wa haki, unaoweza kuamini na ambao unaweza kuthibitishwa" Alisema Miguna.

Mnamo Jumatatu naibu rais William Ruto alipokuwa anahutubia wafuasi aliomba msamaha kufuatia matamshi yaliyotolewa na Linturi mjini Eldoret Jumamosi.