Mwanadada adai kuruhusiwa kutembelea mumewe gerezani kwa ajili ya haki za ndoa

Muhtasari

•Mwanadada huyo ameteta kuwa mumewe anafaa kusalia na haki zake zingine zote ikiwa ni pamoja na haki za ndoa hata kama anatumikia kifungo cha miaka 20 gerezani kwa kosa la mauaji.

•Mnamo 2018 Odhiambo alipatikana na hatia ya kuua wakili Linda Wanjiku, mama wa mtoto mmoja na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20.

Picha ya gereza ya Kamiti
Picha ya gereza ya Kamiti
Image: PATRICK VIDIJA

Mwanamke mmoja amepeleka malalamishi kortini akitaka kuruhusiwa kumtembelea mume wake gerezani kwa ajili ya haki za ndoa.

Haki za ndoa hasa kwa mahusiano ya ngono ni haki ambayo huchukuliwa kuwa ya kisheria kwa kila mtu aliye katika ndoa.

Mwanamke huyo amemshtaki mwanasheria mkuu Paul Kihara akiteta kuwa mumewe, Erastus Odhiambo, anafaa kusalia na haki zake zingine zote ikiwa ni pamoja na haki za ndoa hata kama anatumikia kifungo cha miaka 20 gerezani kwa kosa la mauaji.

Ameteta kuwa amenyimwa haki yake ya kuwa na ukaribu na mumewe na kupata watoto.

"Mlalamishi wa kwanza yuko katika miaka yake ya uzazi na ni hamu yake kuzaa watoto zaidi, kuendelea kuwa mwanamke na sasa anataka kuruhusiwa kutembelea mpenzi wake ili kukidhi mahitaji yake ya kimapenzi," wakili wake alisema.

“Mlalamishi wa kwanza amesoma na kuelewa  Sheria ya Watu walionyimwa Uhuru ya  2014 na anaamini kabisa  kwamba ana haki ya kutembelea mpenziwe kwa ajili ya ngono kwa kuwa mwenzake bado anasalia na haki zote chini ya Kifungu cha 51 cha Katiba

Kukosa kwa mshtakiwa kumpa mlalamishi haki zake na kutomwezesha kufanya ziara kama hizo zilizofafanuliwa hapo juu ni sawa na ukiukaji wa mahitaji yake ya kimsingi kama mwanamke," Wakili huyo alidai.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa Na.4 ya mwaka 2014, iwapo mume au mke ametenganishwa na mwenzake bila sababu za msingi, mhusika anaweza kutuma maombi mahakamani kwa ajili ya kurejeshewa haki za ndoa.

Mahakama ikiridhishwa na ukweli wa taarifa zilizotolewa katika maombi hayo na kukiwa hakuna sababu za kisheria kwa nini maombi hayo yasikubaliwe, inaweza kuamuru kurejeshwa kwa haki za ndoa ipasavyo.

Mnamo 2018 Odhiambo alipatikana na hatia ya kuua wakili Linda Wanjiku, mama wa mtoto mmoja na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20.

Odhiambo alikata rufaa dhidi ya hukumu hiyo, akimkosoa jaji wa mahakama hiyo kwa kumpata na hatia bila ushahidi wa kutosha.

Alidai kuwa hukumu hiyo ilitokana na ushahidi ambao haukuwa thabiti, uliopingana na ambao haukuthibitishwa.

Hata hivyo, majaji wa Mahakama ya Rufaa Fatuma Sichale, P Ouko na W Karanja waliamua kwamba kutokana na jinsi Odhiambo alivyomuua Wanjiku kwa njia ya kikatili, walifikiri kuwa hastahili kifungo cha miaka 20 jela.

Majaji hao walisema Odhiambo alionekana kuwa sehemu ya idadi inayoongezeka ya vijana wanaofurahia utajiri na wanaofikiri kuwa maisha ya binadamu hayana thamani.

Sheria ya Magereza iko kimya kuhusu suala hilo. Haki za ndoa zinaweza tu kufurahia katika mipangilio ya faragha ambayo haipo katika magereza.

Haki hizi zinahusiana kwa karibu sana na haki za afya ya uzazi kama ilivyohakikishwa chini ya Kifungu cha 43 - haki ya kupata familia - na haki ya kuishi chini ya Kifungu cha 26 cha Katiba. Ibara za 24 na 25, hata hivyo, zinaonyesha kwamba haki si kamilifu.

Masharti haya yanaweka kizingiti kigumu sana na utaratibu mgumu wa kuzuia haki.