Kalonzo alemea wenzake katika Oka kwa tiketi ya urais

Muhtasari

• Kulingana na maelezo ya kamati ya kiufundi ya Oka, makamu huyo wa rais wa zamani aliongoza angalau mifumo mitatu ya kusaka mgombeaji.

• Katika pendekezo la kwanza, Kalonzo amependekezwa kuwa kinara wa urais wa Oka huku Musalia akiwa mgombea mwenza wake. 

• Mwigo wa pili unapendekeza kwamba Kalonzo aunganishwe na kiongozi wa chama cha Narc Kenya Martha Karua kama naibu wa rais.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka
Image: MERCY MUMO

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka anaonekana kuwalemea vinara wenzake wa Muungano wa One Kenya kwenye kinyang’anyiro cha kutafuta atakaepeperusha bendera ya muungano huo katika uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu. 

Kalonzo ameongoza mchakato wa kutafuta nahodha wa Oka, akiibuka kidedea zaidi kupata tikiti hiyo inayomezewa mate na vinara wenzake. 

Kulingana na maelezo ya kamati ya kiufundi ya Oka, makamu huyo wa rais wa zamani aliongoza angalau mifumo mitatu ya kusaka mgombeaji.

 Hii ni licha ya vinara wa Oka- Musalia Mudavadi (ANC), Gideon Moi (Kanu), Moses Wetang'ula (Ford Kenya) na Kalonzo - wakirejea Elementaita, Nakuru, leo ( Ijumaa) kukagua ripoti ya kamati ya kiufundi inayoshughulikia utaratibu wa uteuzi wa rais.  

Katika pendekezo la kwanza, Kalonzo amependekezwa kuwa kinara wa urais wa Oka huku Musalia akiwa mgombea mwenza wake. 

Mwigo wa pili unapendekeza kwamba Kalonzo aunganishwe na kiongozi wa chama cha Narc Kenya Martha Karua kama naibu wa rais. Karua ndiye kiongozi wa kongamano la Umoja wa Mlima Kenya ambalo huleta pamoja baadhi ya vigogo wa kisiasa kutoka ngome ya Rais Uhuru Kenyatta.

Viongozi wa OKA Moses Wetang'ula, Kalonzo Musyoka na Gideon Moi wakati wa ibada ya kumuaga Mama Rosebella Jerono Mudavadi katika Kanisa la Friends Church-Quakers mnamo Desemba 16.
Viongozi wa OKA Moses Wetang'ula, Kalonzo Musyoka na Gideon Moi wakati wa ibada ya kumuaga Mama Rosebella Jerono Mudavadi katika Kanisa la Friends Church-Quakers mnamo Desemba 16.
Image: MERCY MUMO

Pendekezo la tatu na la mwisho linapendekeza tikiti ya Kalonzo-Moses Wetang'ula kwa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9. 

Wetang'ula ndiye seneta wa Bungoma. Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi hakuhusika katika uigaji wowote kwa vile anatoka eneo la Rift Valley-eneo ambalo linaonekana kuwa msingi wa kisiasa wa Naibu Rais William Ruto. 

Duru za habari ndani ya kamati ya ufundi ambayo imekuwa katika vikao katika eneo la Elementaita, Nakuru, zilililiambia gazeti la Star kuwa kamati hiyo imefanya kazi yake. 

“Tumehitimisha kazi tuliyopewa na wakuu wetu. Sasa ni juu yao kufanya uamuzi wa mwisho,” Duru zilisema. 

Kamati hiyo inasemekana kuchunguza vigezo mbalimbali katika kufika kwenye safu zilizopendekezwa ikiwa ni pamoja na uwezo wa kila mmoja wa wakuu kupata kura nchi nzima. 

Pia inasemekana waliangalia uwezo wa kifedha wa kila mmoja wa wawaniaji urais wa kufadhili kinyang'anyiro cha urais dhidi ya wapinzani. 

Imeibuka kuwa Musalia huenda hakutuma wawakilishi wake wote kwa kamati ya kiufundi kwa kazi hiyo muhimu ya siku tatu.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO