Majambazi wawili waliokuwa wanatorokea kwa pikipiki wapigwa risasi Nairobi

Muhtasari

•Timu ya wapelelezi waliokuwa wakishika doria waliona pikipiki ambayo nambari yake ya usajili ilikuwa imefichwa kisha mzozo mkubwa kati ya vijana wawili na umati ukazuka.

•Kwingineko, kijana wa umri wa miaka 27 aliteketea hadi kifo usiku wa kuamkia Alhamisi katika kisa cha moto eneo la Lungalunga, mtaa wa Mukuru, jijini Nairobi.

crime scene 1
crime scene 1
Image: HISANI

Washukiwa wawili wa ujambazi walipigwa risasi na kuuawa katika jaribio la wizi katika eneo la Adams Arcade, jijini Nairobi.

Kwa mujibu wa mashahidi na polisi, mauaji hayo yalitokea baada ya polisi kukimbiza gari kwenye barabara ya Lang'ata kufuatia jaribio la wizi ambalo halikukamilika.

Timu ya wapelelezi waliokuwa wakishika doria waliona pikipiki ambayo nambari yake ya usajili ilikuwa imefichwa kisha mzozo mkubwa kati ya vijana wawili na umati ukazuka.

Hilo liliwafanya maafisa hao kutaka kujua kilichokuwa kinaendelea. Vijana hao wawili waliruka juu ya pikipiki na kujaribu kutoroka.

Naibu mkuu wa polisi wa Nairobi James Mugera alisema timu yake iliwafuata hadi kwenye makutano ya Barabara ya Riara-Naivasha, ambapo waliwaua kwa kuwapiga risasi.

"Walikaidi amri ya kujisalimisha, na mmoja akajaribu kuwafyatulia risasi maafisa waliokuwa wakiwaandama. Kwa bahati mbaya walifariki,” alisema.

Miili ya marehemu ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Polisi walisema walipata bastola, simu tatu za rununu na saa ya mkononi aina ya Rolex kutoka kwao.

Mugera alisema wameimarisha operesheni jijini ili kukabiliana na ongezeko la visa vya ujambazi wa kutumia silaha.

Aliwataka wamiliki wa majengo kuweka kamera za CCTV kama sehemu ya juhudi za kudhibiti matukio hayo

 "Kamera kama hizo zinafaa wakati uhalifu unafanywa. Tutafurahi kuona majengo zaidi yakisakinishwa,” alisema.

Kwingineko, kijana wa umri wa miaka 27 aliteketea hadi kifo usiku wa kuamkia Alhamisi katika kisa cha moto eneo la Lungalunga, mtaa wa Mukuru, jijini Nairobi.

Polisi wanasema wanachunguza kubaini ikiwa alijitoa uhai au aliuawa. Nyumba zake mbili  pekee ndizo zilizoathiriwa.

Mwili wake ulipelekwa hadi kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.