Sabina Chege ajipata pabaya baada ya madai ya wizi wa kura

Muhtasari

• Mwakilishi wa kike kaunti ya Murang’a Sabina Chege amejipata pabaya baada ya matamshi yake kuhusu wizi wa kura kuenda mrama

• Sabina Chege aliyazungumza hayo Februari 10 katika mkutano wa kisiasa kwenye kaunti ya Vihiga wakimpigia debe Raila

CHEGE
CHEGE

Mwakilishi wa kike kaunti ya Murang’a Sabina Chege amejipata katika kikaango cha watumizi wa mitandaoni baada ya kunukuliwa akisema kwamba serikali itafanya kila mbinu ili kumsaidia mgombea urais kutoka muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga kushinda uchaguzi wa Agosti 9.

Ghadhabu ya watumizi wa mitandao imepata nafasi nzuri ya kushusha viboko kwa mwanasiasa huyo ambapo wengi wamemkashfu kwa kuzungumza maneno kiholela ambayo yanahatarisha usalama wa taifa haswa kuelekea uchaguzi mkuu.

Sabina Chege, Februari 10 katika mkutano wa kisiasa kwenye kaunti ya Vihiga wakimpigia debe Raila, aliibua madai kwamba kulikuweko na ukweli fulani kuhusu madai yaliyoibuliwa kwamba uchaguzi mkuu wa 2017 ulikumbwa na visa vya wizi wa kura kwa faida ya rais Uhuru Kenya na serikali ya Jubilee na kusema kwamba huenda watalazimika kufanya vivyo hivyo kwa faida ya Raila Odinga.

“Nimesikia watu wakisema kwamba tuliiba 2017. Kuna kaukweli fulani katika hilo. Sasa kama tulifanikiwa kufanya hivo 2017, hata hii tunaweza. Wanafikiria wao ni wajanja,” alisema Chege

Watu wengi nchini wamemkashfu kwa kauli hizo tete na kusema kwamba maneno kama hayo yanaweza kulitumbukiza taifa katika machafuko ya baada ya uchaguzi kama ilivyokuwa baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Wakili tajika Ahmednassir Abdullahi amekuwa mtu wa kwanza mashuhuri kumkashfu Chege kwa madai hayo ya upangaji wa wizi wa kura na kushangazwa kwa kauli hizo kutoka kwa mwanasiasa mwenye uzoefu tena kutoka mrengo wa serikali.