Waziri Yatani kutangaza bajeti [Trilioni 3], matarajio yako ni yapi?

Muhtasari

• Waziri wa fedha anatarajiwa kutangaza bajeti ya kitaifa Alhamisi.

• Itakuwa bajeti ya mwisho kusomwa chini ya uongozi wa rais Uhuru Kenyatta.

Waziri wa fedha Ukur Yatani anatarajiwa kutangaza bajeti ya kitaifa Alhamisi, hii ikiwa bajeti ya mwisho chini ya uongozi wa rais Uhuru Kenyatta.

Kulingana na ripoti kutoka kwa wizara hiyo, bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2022/2023  unaotarajiwa kuanza mwezi Julai itagharimu shilingi trilioni 3.324.

Serikali kuu inatarajiwa kupata mgao wa shilingi bilioni 2.075 pamoja na fungu la shilingi bilioni 2.02 kuelekezwa kwa uongozi mkuu serikalini.

Bunge la kitaifa na mahakama zinatarajiwa kupata shilingi bilioni 38.5 na shilingi bilioni 18.9 kwa usanjari huo.

Pensheni na malipo ya riba kwa deni za nyumbani na za kimataifa zitapata mgao wa shilingi bilioni 864.1 kama ruzuku ya masharti.

Serikali za kaunti kwa upande wao zitapata sehemu yao kutoka kwa shilingi bilioni 370 ambazo ni mgao wa pamoja kutoka kwa serikali kuu pamoja na shilingi bilioni 37.1 kama ruzuku ya masharti.

Wizara ya elimu itapata mgao wa juu zaidi [ bilioni 525.9] ikifuatwa na wizara ya kawi na ile ya usalama kwa shilingi bilioni 368.3 na 203.1 mtawalia.

Wizara ya kilimo itapata shilingi bilioni 63.9 huku wizara ya afya ikipata shilingi bilioni 126.4.

Swali kuu linasalia kuwa mbinu itakayotumika na wizara ya afya kupata fedha hizo. Wizara hiyo imesema kwamba inakusudia kukusanya shilingi trilioni 2.431.

Kenya inatarajiwa kupokea madeni kutoka ughaibuni yenye kima cha shilingi bilioni 275.9 na shilingi bilioni 570.2 kama madeni ya nyumbani.